Unguja. Miradi mikubwa ya kimkakati visiwani Zanzibar inayotajwa kuwa na mchango kwa wananchi na Taifa kwa jumla, imeelezwa kuwa, ni alama ya kukumbukwa mwaka huu.
Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi na ufunguzi wa masoko makubwa ya wajasiriamali ya kisasa ya Jumbi na Mwanakwerekwe.
Mbali na masoko hayo, Serikali tayari imezindua maegesho ya magari ya kwanza ya ghorofa Malindi, Zanzibar. Barabara za mjini na vijijini ni sehemu pia ya miradi itakayoacha alama sio tu kwa mwaka huu lakini kwa miaka mingi ijayo.
Katika masoko hayo, yatanufaisha wafanyabiashara wakubwa na wajasiriamali wadogo wadogo huku wakitengewa Sh46 bilioni kwa ajili ya mikopo.
Mathalani Soko la Mwanakwerekwe ambalo limetumia Sh35.8 bilioni lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 5,000 kwa wakati mmoja.
Pia, Soko la Jumbi lenye uwezo wa kuchukua idadi ya wafanyabiashara 4,000, limegharimu Sh24 bilioni.
Masoko hayo yana sifa zinazofanana yakiwa na maghala, maegesho ya magari, maeneo ya kunyonyeshea watoto kwa mama lishe, maduka, vizimba, mabucha, jiko, sehemu za ibada, machinjio ya kisasa na sehemu ya wafanyabiashara kuhifadhia biashara zao.
Katibu wa Soko la Jumbi, Faki Khatib anasema mradi huo umekuwa mkombozi kwa kuwa, unategemewa na wananchi wengi wa mikoa karibu.
Anasema kwa sasa wajasiriamali na wafanyabiashara wanaendesha biashara zao katika mazingira mazuri na ya kisasa, hivyo kutoa hamasa kwa watu kufanya biashara zao wakiwa na uhakika wa kupata wateja kutoka maeneo mbalimbali.
Khatib anasema awali walikuwa katika mazingira magumu na hakukuwa na eneo linaloeleweka, hivyo kusababisha bidhaa nyingi kuwa katika mazingira magumu huku wakinyeshewa na mvua na kujaa tope.
Mmoja wa wajasiriamali sokoni humo, Halima Sued anasema, “hali ilikuwa tete hata thamani ya vyakula na mbogamboga ilikuwa haionekani kwa sababu ya mazingira mabovu tuliyokuwa nayo.”
Mfanyabiashara katika Soko la Mwanakwerekwe, Rashid Abubakar Haji anasema imani yao baada ya kuboreshewa mazingira watakuza vipato na kupanua uchumi.
“Alhamdulilah, si haba tunapata mazingira mazuri, imani yetu tutafanya biashara tutapanua mitaji yetu, lakini tutakuza vipato na uchumi wa nchi yetu kupitia kodi tunazolipa.”
Baadhi ya wanunuzi wa bidhaa katika masoko hayo wanaeleza kabla na baada ya kujengwa soko hilo.
“Palikuwa hapafai, unafuata mbogamboga hapa unashindwa kuelewa kwa sababu zilikuwa zikipangwa kwenye tope kiafya haikuwa sawa lakini kwasasa hata nafsi inaridhika,” anasema Shanifa Ramadhan mkazi wa Magogoni.
Ujenzi wa barabara za mjini na ndani nao ni miongoni mwa miradi ambayo imeacha alama mwaka huu.
Takribani kilometa 275 za barabara za ndani zimejengwa huku kilometa 100 barabara za mjini zikijengwa, zinazohusisha flyover mbili za Mwanakwerekwe na Amani.
Ujenzi huo sio tu umebadilisha haiba ya mitaa ya Zanzibar bali inatajwa kurahisha usafirishaji na uchukuzi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Oktoba mwaka huu ilizinduliwa Bandari Kavu (ICD) ya kwanza inayotajwa kupunguza msongamano na muda wa makontena kukaa Bandari ya Malindi.
Kwa muda mrefu wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia eneo dogo la Malindi na msongamano vitu vilivyotajwa kuongeza gharama za bidhaa kisiwani humo.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed anasema kwa sasa bandari hiyo inahudumia makontena 120,000 kutoka 80,000 yaliyokuwa yanahudumia kwa mwezi.
Anasema meli zilikuwa zinakaa kwenye nanga kwa siku 42, kwa sasa zinakaa siku 10.
Mwenyekiti wa Wakala wa Forodha, Omar Mussa anasema bandari kavu imeongeza mchango na msukumo mkubwa wa kuondoa makontena katika Bandari ya Malindi na ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana.
“Hizi ni jitihada ambazo tunaona manufaa yake, kwa kweli kilikuwa kilio cha muda mrefu, lakini tumeanza kuona mabadiliko na hii itaongeza uaminifu na watu kufanya shughuli zao kwa uwazi,” anasema.
Akioanisha ukuaji wa uchumi na baadhi ya shughuli hizo, mtaalamu wa masuala ya fedha, Khalid Mussa anasema kuna uhusiano mkubwa wa miradi inayogusa moja kwa moja wananchi na ukuaji wa uchumi Zanzibar.
Khalid anasema iwapo hakuna huduma nzuri zinazowagusa wananchi inakuwa kazi kubwa kufika malengo ya ukuaji wa uchumi.
“Hii miradi ina athari chanya kwa uchumi, kumbuka huwezi kujenga uchumi kwa kutengeneza vitu ambavyo haviwagusi moja kwa moja wananchi kwa sababu utakuwa unalenga kundi fulani na kundi lingine litabaki nyuma lakini kwa mazingira haya kila mmoja anaguswa kwa namna yake,” anasema Mussa.
“Unapotengeneza maeneo ya kupata huduma kwa urahisi, inapunguza hata muda na gharama, inawezekana kwa jicho la kawaida isieleweke lakini kitaalamu ipo hivyo.”
Kwa mujibu wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, mambo yote anayoyatamka hadharani juu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo sio porojo za kisiasa bali ni dhamira yake ya kweli ya utekelezaji.
Licha ya kuwapo watu wanaotaka kumkatisha tamaa, anasema hatarudi nyuma badala yake anaangalia utekelezaji wa miradi ya maendeleo waliyoitoa kwa wananchi wakati anaomba kura mwaka 2025.
Akiweka jiwe la msingi katika flyover Mwanakwerekwe juzi. anasema Serikali imejipanga na inatafuta fedha kutekeleza miradi mikubwa na watahakikisha Zanzibar inajengwa kila kona.