Rais mteule Donald Trump ameahidi “kukomesha wazimu wa watu wa jinsia tofauti” katika siku ya kwanza ya urais wake, wakati Warepublican — wanaotarajiwa kudhibiti mabunge yote mawili pamoja na Ikulu ya Marekani — wakiendelea na juhudi zao za kupinga haki za LGBTQ.
“Nitasaini amri za kiutendaji kukomesha ukeketaji wa kijinsia wa watoto, kuondoa watu waliobadili jinsia jeshini na mashuleni kuanzia shule za msingi, za kati hadi za sekondari,” rais mteule Trump alisema katika hafla ya vijana wa kihafidhina mjini Phoenix, Arizona.
Aliahidi pia “kuwazuia wanaume kushiriki michezo ya wanawake,” na kuongeza kuwa “itakuwa sera rasmi ya serikali ya Marekani kwamba kuna jinsia mbili tu, ya kiume na ya kike.”
Soma pia:Marekani yaahirisha mkutano wa VVU/UKIMWI nchini Uganda kufuatia sheria tata ya LGBTQ
Akizungumza kwenye mkutano wa AmericaFest katika jimbo la mpakani aliloshinda kwa urahisi katika uchaguzi wa Novemba, Trump aliahidi hatua za haraka dhidi ya “uhalifu wa wahamiaji,” kuahidi kutangaza magenge ya dawa za kulevya kuwa mashirika ya kigaidi ya kigeni, na kusisitiza tena nia yake ya kurejesha udhibiti wa Marekani katika Mfereji wa Panama.
Masuala ya watu wa jinsia tofauti yamekuwa yakitikisa siasa za Marekani katika miaka ya hivi karibuni, huku majimbo yanayoongozwa na Democrats na Republicans yakichukua mielekeo tofauti kuhusu matibabu ya kiafya na vitabu gani vinavyohusiana na mada hiyo vinaruhusiwa katika maktaba za umma au za shule.
Wiki iliyopita, wakati Bunge la Marekani lilipokubali bajeti yake ya kila mwaka ya ulinzi, ilijumuisha kifungu cha kuzuia ufadhili wa baadhi ya huduma za uthibitisho wa kijinsia kwa watoto wa wanajeshi waliobadili jinsia.
Katika hotuba yake ya Jumapili, ambayo ilionekana kama sherehe ya ushindi, Trump alitoa ahadi nyingi kwa muhula wake wa pili — na kuchora taswira ya giza kuhusu miaka minne iliyotangulia chini ya Rais Joe Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris, ambaye alimshinda katika uchaguzi wa 2024.
“Tarehe 20 Januari, Marekani itafungua ukurasa mpya milele baada ya miaka minne mirefu na ya kutisha ya kushindwa, kutokuwa na uwezo, na kushuka kwa taifa, na tutaanzisha enzi mpya ya amani, ustawi, na ukuu wa kitaifa,” Trump alisema, akizungumzia kuapishwa kwake.
“Nitamaliza vita nchini Ukraine. Nitakomesha machafuko katika Mashariki ya Kati, na nitaizuia, naahidi, Vita vya Tatu vya Dunia.” Aliongeza: “Enzi ya dhahabu ya Marekani iko karibu nasi.”
Hata hivyo, rais mteule bado hajafafanua hadharani jinsi anavyopanga kumaliza haraka vita nchini Ukraine au kuleta amani Mashariki ya Kati.
Atishia kuchukua udhibiti wa mfereji wa Panama
Lakini kwa lugha ya ukali ambayo mara nyingine hutumia hata dhidi ya washirika wa Marekani, Trump alisema Jumapili kwamba serikali ya Panama “haijatutendea haki” katika uendeshaji wao wa Mfereji wa Panama.
Soma pia: Marekani yawaonya raia wake walio ugenini kuhusu uwezekano wa matukio ya LGBTQ kushambuliwa
Alisema awali kuwa ada za matumizi ya mfereji huo — ambao ujenzi wake ulianzishwa na Ufaransa na kukamilishwa na Marekani — ni “za kipuuzi.”
Na akaongeza Jumapili kuwa ikiwa misingi ya mkataba wa miaka ya 1970 uliowapa Panama udhibiti kamili wa mfereji huo haitafuatwa, “basi tutadai” kwamba urejeshwe kwa Marekani “kwa ukamilifu, haraka, na bila maswali.”
Maelfu ya meli hupitia mfereji huo muhimu wa Amerika ya Kati kila mwaka, na kuufanya kuwa muhimu kwa biashara ya Marekani na ya kimataifa.
Rais mteule, ambaye mara kwa mara huwalaumu wahamiaji kutoka Amerika ya Kusini kwa matatizo ya dawa za kulevya nchini Marekani, alirejea ahadi yake ya kuanza mara moja “operesheni kubwa zaidi ya kufukuza wahamiaji katika historia ya Marekani” pindi tu atakapoingia madarakani, na baadaye akaenda mbali zaidi, kwa kusema atatangaza mara moja magenge ya dawa za kulevya kama mashirika ya kigaidi ya kigeni.
“Mtandao huu wa uhalifu unaoendesha shughuli zake kwenye ardhi ya Marekani utavunjwa, wahusika watatolewa nchini na kuangamizwa,” Trump alisema.
Wakati wa muhula wake wa kwanza mnamo 2019, baada ya mauaji ya raia tisa wa Marekani kutoka jamii ya Wamormoni nchini Mexico, Trump aliahidi kuyatangaza makundi ya dawa za kulevya ya Mexico kuwa mashirika ya kigaidi.
Lakini alisitisha mpango huo kufuatia ombi la rais wa Mexico wakati huo, Andres Manuel Lopez Obrador.