Simulizi dereva aliyewaendesha marais watatu

Mara nyingi, kuna watu wanaoenziwa na kutuzwa nchini kwa kufanya mambo mbalimbali mazuri.

Lakini wengi wao huwa wasomi wabobezi, wanasiasa au wanamichezo na wasanii wachache.

Si aghalabu kuona watu wanaoonekana wa kada ya chini wakitukuzwa kwa lolote japo wanafanya mambo makubwa. 

Mmoja wao ni Ismail Mputila, dereva aliyewaendesha marais watatu kwa takriban miaka 25.

Awali  alikuwa  Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, kwa miaka mitano – 1980 hadi alipong’atuka 1985; wa pili, Ali Hassan Mwinyi kwa miaka kumi – 1985 – 1995 na tatu Rais Benjamin Mkapa, pia kwa miaka kumi – 1995 – 2005. Alikuwa, hata hivyo, anasaidiana na madereva wenzake, kila inapobidi.

“Ilionekana kama nitamuendesha Rais Kikwete baada ya uchaguzi wa mwaka 2005…wakaniacha nami nikafurahi kwa vile nilibakiza miaka miwili tu nistaafu…”, anasema Mputila, aliyezaliwa mwaka1947 na ambaye sasa ana umri wa miaka 77.

Siyo watu wengi, hata wasomi, wanaoweza kuyafanya aliyoyafanya Mputila aliyestaafu mwaka 2007.

Ofisa mmoja wa ngazi ya juu wa  kitengo cha ulinzi wa Rais, aliyefanya kazi tangu enzi za awamu ya kwanza, anamkumbuka Mputila na utendaji wa kazi zake.

Mputila alizaliwa Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Alianza shule ya msingi, Bunju, akamalizia  Kigamboni. Akaajiriwa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, Ubungo, jijini Dar es Salaam mwaka 1970, kilichokuwa kinaajiri vijana waliomaliza shule ya msingi.

Aliwekwa kwenye idara ya kufuma nyuzi kuwa kitambaa.

‘’Sikuipenda kazi, ilikuwa ya harubu kutokana na vumbi la pamba linalotimka pale. Nikaamua kuacha kazi na kujifunza udereva…”, anasema.

Ilikuwaje mpaka Mputila, akaingia katika kazi ya kuwaendesha viongozi wakuu?  Anaeleza:  “Baada ya kufuzu udereva mwaka 1971, nikaajiriwa na Emti Depo (Motor Transport Department – M.T. Depot, kitengo cha Serikali kilichokuwa kinashughulikia usafiri wa magari serikalini bararabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam).

‘’Nikawa dereva wa kawaida, lakini baadaye nikajikuta nimehamishiwa Ikulu…” Ilikuwa hivi. Ikulu,  wizara au idara mbalimbali za Serikali zinapohitaji huduma ya usafiri, magari au madereva, hupata huduma hiyo kutoka M.T. Depot, kwa kuazima au moja kwa moja. “Madereva wenzangu wazoefu pale M.T. Depot, wakimuona ofisa wa Ikulu amefika kutaka dereva huwa wanajificha kwa vile wengi wao walikuwa hawapendi kufanya kazi kwenye jumba kuu kutokana na kuona kuwa kazi ya huko ni ya sulubu…”

Ismail Mputila akiwa na gari aina ya Mercedes Benz, alilokuwa akilitumia kuwaendeshea Marais.

Anaendelea kusimulia: “Siku moja, Januari 1972, dereva mkuu wa Ikulu, Saidi Tanu, alipokuja M.T. Depot kutaka dereva akamshikie dereva mwingine wa Ikulu. Mimi nilikuwa nimezubazubaa tu, sijui chochote, hivyo nikapatikana mimi na kuambiwa kuwa nitakwenda kufanyakazi Ikulu kwa kuazimwa, kwa muda. Nikasema mimi siyaelewi mazingira ya Ikulu, lakini nikaambiwa kuwa kinachohitajika zaidi ni kuwa na nidhamu. Nilivyofika Ikulu nikawekwa kwenye kundi la madereva,  nikapewa gari aina ya Peugeot 404 na nikakabidhiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, nimuendeshe…Hivi ndivyo nilivyoingia Ikulu…”.

Anasema mwaka 1975 aliteuliwa kwenda Chuo cha Wizara ya Ujenzi Morogoro kusomea stadi zaidi za udereva kwa miezi mitatu na akarudi tena Ikulu kuwaendesha viongozi wengine mbalimbali.

 “Mwaka 1978, nikachaguliwa kumuendesha Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe (Rais wa pili wa Zanzibar, baada ya kuuawa kwa Rais wa Kwanza, Abeid Amani Karume), kila akija Dar es Salaam kwa vikao. Nilimwendesha Jumbe kwa takriban mwaka moja hivi,” anasema.

Anakumbuka kuwa alipokuwa Ikulu akafundishwa kuendesha gari la kifahari, Rolls Royce, ambalo wakati huo, lilikuwa linatumiwa Ikulu kupokea marais kutoka nje ya nchi wanaokuja kutembelea Tanzania.

Gari hilo lililotengenezwa Uingereza, ni la modeli ya miaka ya 1930, liliachwa nchini baada ya Uhuru, likiwa limetumiwa na Gavana wa mwisho wa Tanganyika, Sir Richard Turbull. Sasa hivi liko Makumbusho ya Taifa.

Anasema baada ya dereva mwingine wa Ikulu, Hassan Hamisi kustaafu mwaka 1980, ikabidi wamtoe kwenye Rolls Royce ili amwendeshe Mwalimu Nyerere.  Hapo ndipo  Mputila alipoanza kumuendesha Rais Nyerere na kisha  marais waliofuata.

 “Nilidhani Mwalimu alipong’atuka mwaka 1985, ningerudi  kwenye kundi la madereva wanaosubiri kupangiwa kazi, hapana. Ofisi ikaniteua tena niwe dereva wa marais…”.anaeleza.

Mputila anasema kila kiongozi aliyemwendesha, alikuwa na haiba yake kama ilivyo katika aina  za uongozi wao.

Hata hivyo,  anakumbuka zaidi tabia ya Mwalimu Nyerere  na Mzee Mwinyi ya  kutokuwa na makuu,  kujishusha na kutojikweza, sambamba na uwazi na ukweli aliyokuwa anayo Mkapa.

Kwa Mwalimu Nyerere  anakumbuka tukio la kuhudhuria kwenye shughuli ya dua (hitma) ya Sheikh Mohammed Ramiya, Bagamoyo. Sheikh Ramiya alikuwa mashuhuri sana kataka harakati za TANU za kupigania uhuru.

Katika shughuli hiyo, Mzee Mputila anasimulia kuwa  Mwalimu akiwa Rais, alipiga goti na kukaa kwenye jamvi  kushiriki na waombolezaji na waumini kwa kuchangayika nao kwenye kisomo na wakati wa kula.

Anamkumbuka Mzee Mwinyi kuwa mara kwa mara wakati anamuendesha kwenda shambani kwake  Mwanambaya, wilayani Mkuranga, alikuwa akisimama kwenye msikiti wowote ulio karibu wakati wa sala na kuchanganyika na waumini katika ibada,  bila ya kujali itifaki maalum ya kirais.

“Kwa Rais Mkapa namkumbuka kuwa hasiti kuniambia kama nakwenda spidi kali nipunguze au nakwenda taratibu sana niongeze kasi,” anaongeza kusema.

Mputila anasema kuwa hakuwa na mazungumzo na abiria wake hao aliokuwa anawaendesha na hata walinzi wao wa karibu, labda pale tu atakapoulizwa swali na Rais na kumjibu. “Ndiyo aina moja ya nidhamu hiyo niliyoaambiwa niwe nayo ninapowaendesha viongozi wakuu,” anasema.

Tukio moja baya analolikumbuka ni ajali mbaya ya Mwanza katika kipindi cha mwanzo cha Rais Mkapa. Anasema walitoka mjini kuelekea nje ya mji katika ziara, lakini ghafla  kwenye msafara barabarani wakaona basi kubwa linateremka kwa kasi kutoka kwenye mwinuko, nusura ligonge gari ya Rais.

 Akajitahidi kulikwepa  basi hilo likawaparamia baadhi ya wananchi kando ya barabara waliokuwa wakishuhudia msafara wa Rais na kutumbukia kwenye gema.

“Ilikuwa ni bahati tu tukanusurika…nilipatwa mshtuko nikashindwa hata kundelea kuendesha, nikampisha dereva mwenzangu mwingine. Wakubwa wangu wakaamua ziara isimame turudi mjini,” anasimulia.

Anasema katika ajali hiyo, kulikuwa na baadhi ya vifo na majeruhi, kwa mujibu wa kumbukumbu zake. Kwa sasa Mputila anasema hahitaji tena kuendesha gari lolote, kwani ameamua kupumzika nyumbani kwake wilayani Kinondoni.

Related Posts