Yacouba aivutia kasi Simba SC

TABORA United bado ina hasira za kichapo cha mabao 3-0 ilichopewa na Simba katika mechi ya duru la kwanza ambacho iliwakosa mastaa wake wa kigeni kutokana na ishu za vibali, na sasa inasubiri kwa hamu mchezo wa marudiano utakaopigwa mjini Tabora ulioahirishwa na kuelezwa ni furaha kwa timu hiyo kwani inatoa muda kwa majembe yao kupona vizuri.

Mmoja ya wachezaji waliokuwa wakiipa wasiwasi Tabora ni Yacouba Songne aliye majeruhi, lakini imeelezwa anaendelea kupambana ili arudi uwanjani akiwa fiti zaidi na kuchekelea taarifa za kuahirishwa kwa mchezo wa marudiano na Simba uliokuwa upigwe mwishoni mwa mwezi huu.

Yacouba amekosa mechi mbili zilizopita dhidi ya Azam waliyoifunga 2-1 na ile ya Coastal Union iliyoisha kwa sare ya 1-1 baada ya kuumia goti katika mchezo walioichapa KMC 2-0 ugenini akitumika kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, akifunga bao moja la utangulizi kabla ya kutolewa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Yacouba alisema amefurahishwa na mchezo dhidi ya Simba kusogezwa mbele ambapo anatamani kucheza dhidi ya Wekundu hao.

Yacouba alisema, kiu yake inatokana na mchezo wa kwanza baina ya timu hizo alioukosa kutokana na kukosa vibali ambapo timu yake ilipoteza kwa mabao 3-0 matokeo yaliyoifanya kuanza ligi vibaya.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga na Ihefu alisema anaamini ili awe bora anatakiwa kufanya makubwa katika mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, huku Tabora ikiwa imeshazichapa Yanga na Azam na kutoka sare ya Singida BS zinazounda Nne Bora ya Ligi Kuu kwa sasa.

“Mechi ya kwanza niliikosa nadhani mnakumbuka mambo yaliyotokea, lakini nilipata wasiwasi kama na hii ya pili nitaikosa, sasa ilivyosogezwa mbele nimefurahi sana nadhani nitakuwa nimepona sawasawa,” alisema Yacouba na kuongeza;

“Simba ni timu kubwa, ukitaka uonyeshe ubora unatakiwa kufanya makubwa katika mechi kama hizi unazokutana nazo, namshukuru Mungu maendeleo yangu ni mazuri sana kwasasa nazidi kuimarika nitarudi kuiongezea nguvu timu yangu.”

Mshambuliaji huyo aliongeza ana furaha na wachezaji wenzake ambao wakati akiwa nje wameipigania Tabora United na haijapoteza mechi yoyote ikishinda mchezo mmoja na kutoa sare moja na kushinda moja.

“Wachezaji wenzangu ni wanajeshi wazuri sana nawapongeza sana, hizi mechi mbili tulizocheza nikiwa sipo wameipigania sana timu yetu,” alisema.

Aliongeza; “Tuna kocha mzuri pia ambaye ndani ya muda mfupi amefanikiwa kutuunganisha vizuri na timu inacheza kikubwa.”

Yacouba ndiye anayeongoza kwa ufungaji wa mabao kwa timu hiyo akifungana na Offen Chikola kila mmoja akiwa na manne, huku Heritier Makambo akifuata akiwa na matatu na kuifanya timu hiyo ishike nafasi ya tano ikicheza mechi 15 na kushinda saba, ikitoka sare nne sawa na ilizopoteza na kufunga mabao 19 na kufungwa kama hayo huku ikivuna jumla ya pointi 25.

Related Posts