KLABU ya Namungo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa winga wa Coastal Union, Issa Abushehe ‘Messi’, baada ya nyota huyo kuvunja mkataba wake wa mwaka mmoja na miezi sita uliobakia na KVZ ya visiwani Zanzibar.
Nyota huyo alijiunga na KVZ msimu huu akitokea Biashara United ya mkoani Mara inayoshiriki Ligi ya Championship ingawa ameitumikia kwa miezi sita tu, kisha kuamua kuvunja mkataba wake uliobakia kwa makubaliano ya pande mbili.
“Nilisaini mkataba wa miaka miwili lakini nimefikia uamuzi wa kuuvunja kwa makubaliano ya pande mbili, kwa sasa nipo huru kwa sababu nahitaji kwanza kupumzika kabla ya kwenda timu nyingine ambayo nitaamua kujiunga nayo,” alisema Messi.
Kuhusu Namungo, Messi alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu hakuna dili lililokamilika, lakini ikiwa kila kitu kitakamilika ataweka wazi na mashabiki wake watajua timu atakayoichezea katika dirisha hili dogo.
Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman alisema bado hawajakamilisha usajili wa mchezaji mwingine zaidi ya waliowatangaza na kama watafanikisha wengine wataweka wazi, japo taratibu za kuboresha kikosi hicho katika dirisha hili bado zinaendelea.
Messi ni miongoni mwa wachezaji wenye vipaji vikubwa ambapo wakati akiwa na Coastal Union alipata dili la kujiunga na Al Mokawloon Al Arab inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri, japo alirejea nchini na kujiunga na Biashara United ya mkoani Musoma.
Endapo dili hilo litakamilika, Messi ataungana na Derrick Mukombozi na Emmanuel Charles waliorejea tena ndani ya kikosi hicho, beki wa kati Daniel Amoah aliyewahi kutamba na Azam FC na kiungo, Najim Mussa aliyetokea Singida Black Stars.