MAKUNDI KUITAFUNA CCM NYAKATO, WAMBURA AKIAHIDI MABATI BANDO MBILI UJENZI OFISI YA MTAA


NA BALTAZAR MASHAKA, ILEMELA

MJUMBE wa Baraza la Wazazi CCM Mkoa wa Mwanza, Alfred Wambura (Trump) amesikitishwa na makundi na ubaguzi unaoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi kata ya Nyakato, wilayani Nyamagana.

Wambura ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kumpongeza Menyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Majengo,Kata ya Nyakato Desudedit Malunde (CCM),alionesha masikitiko hayo,leo huku akiwapongeza wananchi kwa kuchagua Malunde kwa vipindi vitatu mfululizo.

Amesema katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024,wapo wana CCM wengi waliomba kupendekezwa na Chama ili wagombee nafasi hizo za uongozi katika mitaa yao lakini ni mmoja tu aliyepata nafasi ya kuwakilisha Chama kila mtaa kwa nafasi ya mwenyekiti.

“Tunagombana ndani lakini baada ya kuteuliwa mmoja tubadilika na kuwa kitu kimoja,hiyo ndiyo demokrasia ndani ya Chama Cha Mapinduzi.Hata mimi niliwahi kugombea nikashindwa,nilikubali matokeo na kumuunga mkono,sasa CCM Kata ya Nyakato hali ni tofauti,”amesema Wambura.

Amesema kuwa anafurahishwa na wananchi kwa kumchagua Malunde kwa kipindi cha tatu na kuonya,kamwe makundi ya uchaguzi yakiendekezwa yatakigharimu Chama na kukwamisha maendeleo,wenye nia na dhamira ya kuendeleza makundi ilhali uchaguzi umekwisha wajitathmini kwa maslahi mapana ya CCM na maendeleo ya wananchi.

Mjumbe huyo wa Barazala Wazazi ameonya makundi yakiendekezwa yatasababisha mpasuko mkubwa ndani ya Chama na kutoa mwanya kwa wapinzani, hivyo wenye makundi wayavunje kwani uchaguzi umekwisha na walioshindwa wajipange upya kwa uchaguzi ujao.

Akijibu risala ya Mtaa wa Majengo iliyosomwa na Veronica Mtiro, ikieleza changamoto ya ukosefu wa vifaa vya ujenzi wa ofisi ya serikali ya mtaa huo,vinavyogharimu sh.milioni 25 Wambura ameahidi kutoa bandol mbili za mabati na saruji mifuko 10.

“Mwenyekiti nimeshikwa na uchungu kwa hili nililoliona, umeachwa yatima na mimi nitakuunga mkono, nitachangia mabati bandol mbili na saruji mifuko 10,”ameahidi Wambura.

Ujenzi huo wa ofisi ya mtaa,tayari ulishaanza kwa nguvu za wananchi ambapo Mbunge wa Ilemela, Dkt. Angelina Mabula,alichangia matofali yenye thamani ya zaidi ya sh.1,000,000.

Naye Masatu Mukabe mmoja wa wazee wa Kata ya Nyakato,amesema licha ya ushirikiano anadhani bado kuna mgawanyiko na watakuwa wanajidanganya, wakigawanyika ndani ya CCM watatengeneza mpasuko mkubwa.

Ameshauri wenye makundi yaliyosigana sababu ya uchaguzi kuungana kwa maslahi ya CCM na maendeleo ya wananchi wa Majengo huku akimtaka mwenyekiti na wajumbe, kuwasikiliza wananchi na wanachama pamoja na kutatua kero zao.
Kwa upande wake,Malunde amewashukuru mabalozi kwa kazi kubwa na wananchi kwa imani yao kwa iliyowasukuma kumchagua kwa awamu ya tatu,kwamba hana cha kuwalipa zaidi ya maendeleo ambayo ni dira yake.Katika mkutano huo wa kupongeza mwenyeiti na wajumbe, ahadi mbalimbali za vifaa vya ujenzi wa ofisi zilitolewa ili kukamilisha ujenzi huo.

Related Posts