Shule zinavyopuuza agizo la kutoendelea na masomo msimu wa likizo

Wakati wanafunzi wakiwa likizo tangu Desemba 7, mwaka huu baadhi ya shule zimeendelea kuwanoa wanafunzi wake, hoja ikiwa mwakani wanakabiliwa na mitihani ya Taifa.

Wanafunzi hao ni wale wa darasa la tatu ambao mwakani wataingia la nne na darasa la sita ambao mwakani wataingia la saba.

Hata hivyo wakati hali ikiwa hivyo, Serikali kupitia Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa, imsisitiza shule kuheshimu ratiba za likizo, huku akionya watakaobanika kuendelea kufundisha watoto, kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Walichosema wazazi, wanafunzi

Mmoja wa wazazi ambaye hakutaka jina ake litajwe gazetini, anasema mtoto wake anasoma darasa la sita, katika shule moja ya Serikali iliyopo Chanika, tangu wenzao wamefunga shule yeye hajafunga.

Anasema wazazi waliambiwa wawaache waendelee kwenda kwa kuwa wanawaandaa kwa ajili ya darasa la saba na pindi watakapofungua, watakuwa na mtihani wa wilaya.

“Imebidi nikubali aende kwa kuwa usipokubali wenzake wao wanaendelea kusoma na mwalimu harudi nyuma,’’ anasema.

Mzazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Anna, anasema kinachosikitisha ni kwamba kila wakienda wanapaswa kwenda na Sh1,000 na kuhisi kuwa huenda ni mradi wa mtu.

“Hivi kweli kama walimu wameamua kukimbizana na muda na lengo ni kutaka watoto wafaulu, basi wangejitolea tu, lakini unapomwambia kila mtoto aende na Sh1,000 na wapo zaidi ya 200, huo ni mradi wa mtu.

“Lakini kwa kuwa nasi tunataka watoto wetu wasome hatuna budi kukubali maana ukikataa mwenyewe utaonekana mjeuri na mtoto wako atatengwa,’’ anasema na kuongeza:

“Nadhani Serikali inapotoa katazo, isiishie kulitoa kwenye makaratsi bali iwe inafanya na doria za kushtukiza kwenye kwenye shule, ili kukomesha vitendo hivyo kwa kuwa sio wazazi wote tunapenda hii hali.

Maliki Kivamwo mkazi wa Kigamboni, anasema ameshindwa kumpeleka mtoto wake likizo kwa bibi yake kutokana na kutakiwa kwenda shule.

“Wengine huwa tunapenda kuwapeleka watoto kwa ndugu kipindi hiki cha likizo ili wakawajue na ndugu zao wengine, maana kuna leo na kesho, lakini hiyo nafasi anaipata wapi kama ni kusoma tu kuanzia Januari hadi Desemba” anahoji.

Salma Abdi, mkazi wa Kimara, anasema imefika mahali mzazi kwa mwaka mzima unashindwa kujua hata tabia za mtoto wako, kwa kuwa mmekuwa watu wa kupishana, yeye akienda shule wewe kazini, lakini kama kungekuwa na likizo pia angeamua kuchukua likizo walau wiki moja.

“Mimi nina mtoto mmoja, na ndio huyu anaingia darasa la nne, ina maana kuanzia sasa mpaka mwakani Oktoba, sitakuwa na muda mzuri wa kukaa na mtoto wangu zaidi ya Jumapili.

‘Hii si sawa tunaomba Serikali ikazie jambo hilo la watoto kutakiwa kwenda shule kipindi cha likizo, kwa kuwa tunajua hawakuweka likizo kwa bahati mbaya,’’ anasema.

Gabrela Ezekiel mkazi wa Tegeta, anasema mtoto wake aliyekuwa anasoma shule ya kutwa, ilipofika Oktoba tu shule iliwataka wote wanaoingia darasa la saba mwakani kwenda kukaa bweni na kuelezwa watawaruhusu siku mbili kwenda kula sikukuu ya Krismass na baada ya hapo watarejea tena shule Januari 3,2025.

Mmoja wa wanafunzi katika shule moja(jina tunalihifadhi), anasema ambao hawaendi shule wameambiwa wakifungua watachapwa fimbo tatu kila mmoja.

Hata hivyo, anasema wakati darasani kwao wakiwa wanafunzi 98, mpaka sasa wanaoenda ni 77, na kila wiki wanakwenda na Sh5,000 na wameambiwa watafunga shule wiki ya tatu ya Desemba.

Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa, anasema waraka wa watoto kutokwenda likizo uliotolewa mwaka 2023 upo palepale na kuhoji hao wanaendelea kuwaambia watoto waende shule wanakiuka maagizo hayo.

Dk Mtahabwa, anasema hawatasita kuwachukulia hatua yoyote wanaofanya hivyo kwa kuwa Serikali imelikataza hilo kwa nia njema.

Anasema haiwezekani mtoto kuanzia Januari hadi Desemba kusoma tu makaratasi wakati kuna shughuli nyigine za kujamii anatakiwa kuzifanya na kujifunza.

“Tukibaini yeyote anayeruhusu mtoto kwenda shule katika kipindi hiki, iwe shule binafsi au Serikali tutamchukulia hatua. ‘Lakini pia hao wanaofanya hivyo wajue wathibiti ubora wetu wapo mtaani, hivyo endapo watamkuta hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake,”anasema Kamishna huyo.

Mwalimu wa lugha na mhadhiri mwandamizi wa saikoljia ya walimu katika Chuo Kikuu kishiriki cha Ualimu(DUCE), Dk Mabula Nkuba anasema kwa wazazi wasioelewa, wataona kama watoto wao wanaonewa.

Anatoboa siri kwamba, walimu wanalazimika kufanya hivyo kwa kuwa kwenye familia nyingi watoto hawana kazi. Wengi wanashinda tu nyumbani kukaa na kuangalia runinga.

“Hivyo walimu wanalalamika wanaporudi Januari mambo yote yanakuwa yamefutika hivyo kwa kutaka waende shule, walimu wanapunguza muda wa wao kuangalia katuni,”anasema mhadhiri huyo.

Sababu nyingine anasema ufanyaji tathimini wa Serikali katika masomo hivi sasa umebadilika hali inayochangia shule nyingi nazo kubadili mfumo wa ufundishaji.

“Ni kutokana na hilo hata yale masomo ya ziada jioni kwa sasa yametengenezwa sio kwa kusaidia wanafunzi ambao hawajaelewa, bali kukimbizana na muda wa ufundishaji.

“Kwa sasa kuna mitihani mingi inafanyika na hivyo kuna muda wa kufundisha.Mfano kuna mitihani ya shule za Serikali, za binafsi, kata kwa kata, bado wilaya,ndio maana walimu nao wanaona watafute muda mwingine wa kufundisha,’’ anaeleza.

Nye mhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu cha Iringa, Valerius Haule, anasema ubongo wa mtoto unahitaji kupumzika ili kuanza tena kujifunza mambo mapya, ndio maana kunakuwa na kalenda, akieleza kuwa kusoma mfululizo ni kuchosha ubongo wa wanafunzi.

“Kwa bahati mbaya sana watoto wetu kwa utamaduni wa Kiafrika, hatuwapi msingi mtoto wa vitu gani vya kufanya wanapokuwa nyumbani, hivyo tunawaacha huru sana kufanya mambo mengine yasiyowajenga na ndio maana wazazi wengine wanaona bora waende shule.

‘’Uhuru huo ukipitiliza unakuwa na athari kubwa kwa mtoto, hivyo ni suala la mzazi kupima nini anataka kufanya kwa mtoto wake kwani kuna njia ya kuwapangia kazi za kufanya au ratiba ikiwemo kujikumbusha mara chache yale aliyoyasoma ili shule zikifunguliwa asisahau kabisa kile alichofundishwa,’’ anasema.

Hata hivyo, anasema anachokiona kwa sasa kwa wanafunzi kutakiwa kwenda shule ni twisheni mbadala ambayo iliwahi kupigwa marufuku kwa kuwa ukweli ni kwamba hawaendi kusoma bure.

Related Posts