KASI ya Simba na Yanga katika Ligi Kuu Bara katika mechi za hivi karibuni Lihi Kuu Bara, imemshtua Kocha wa Azam, Rachid Taoussi na kuwataka mastaa wake kutofanya makosa kwenye mechi zijazo ili kuendelea kuleta ushindani msimu huu.
Kitendo cha Simba kuifunga Kagera Sugar mabao 5-2, huku Yanga ikiifunga Tanzania Prisons mabao 4-0 kimeifanya Azam kushushwa hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 33 baada ya kucheza michezo 15 huku Simba ikiongoza na alama 34 ikifuatiwa na Yanga yenye 33.
Akizungumza na Mwanaspoti, Taoussi alisema maendeleo yao sio mabaya hadi sasa katika ligi, japokuwa wana jukumu kubwa wanalokabiliana nalo katika michezo ya raundi ya pili ili kuendeleza ushindani na wapinzani wao.
“Tumemaliza mzunguko wa kwanza tukiwa sehemu nzuri kwa maana hatujapishana sana pointi na washindani wetu. Kikubwa ni kuendelea kuongeza umakini katika michezo yetu ijayo ambayo itatusaidia kupunguza pengo lililopo na wenzetu,” alisema.
Taoussi ambaye kitaaluma ni daktari aliongeza kuwa hadi sasa hakuna timu yenye uhakika wa kuendelea kushika nafasi ya kwanza ndio maana kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara, hivyo wataendelea kuongeza nguvu kwenye kila mchezo wanaocheza.
Tangu Taoussi ateuliwe kuiongoza Azam Septemba 7, mwaka huu akichukua nafasi ya Msenegali, Yousouph Dabo, ameiongoza timu hiyo katika michezo 14 ya Ligi Kuu Bara, akishinda 10, sare miwili na kupoteza miwili.
Kwaujumla Azam imecheza michezo 15, ikishinda 10, sare mitatu na kupoteza miwili, ambapo imefunga mabao 22 na kuruhusu saba, ikiwa nafasi ya tatu na pointi 33, sawa na Yanga iliyopo ya pili zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Azam iliyobeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara moja msimu wa 2013-2014 tangu ilipoanza kushiriki ligi hiyo mwaka 2008, imekuwa ikipambana kubeba tena mara nyingine lakini inakutana na upinzani mkubwa kutoka kwa Simba na Yanga zinazopokezana taji hilo kwa muda mrefu.