Mashujaa malengo yametimia | Mwanaspoti

MECHI 15 za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara zimempa mwanga Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Bares’ aliyedai watahakikisha wanakuwa bora zaidi ili kumaliza nafasi tano za juu.

Mashujaa baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza kwa kucheza mechi 15, imeshinda nne, sare saba na vipigo vinne, ikifunga mabao 13 na kuruhusu 11 ikikusanya pointi 19 zilizoiweka nafasi ya saba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bares alisema mzunguko wa kwanza wamefanikiwa licha ya kudondosha pointi nyingi kwa kuambulia sare kwenye mechi saba, lakini si haba kwa sababu malengo ni kuwa nafasi nzuri.

“Mzunguko wa kwanza tumefikia malengo sio kwa idadi ya pointi tu, bali nafasi tuliyopo ndio yalikuwa malengo yetu. Kilichobaki ni kuchanga karata zetu vizuri mzunguko wa pili ambao tunatarajia kuwa na ugumu kutokana na kila timu kuutumia kujiweka kwenye nafasi,” alisema.

“Mzunguko wa pili ni wa lalasalama timu nyingi zitarudi kwa nguvu kupambania hatima ya kucheza msimu ujao na pia kujiweka kwenye nafasi nzuri za juu kama kutwaa taji, mshindi wa pili hadi wa tano. Tunatarajia vita kali kwani timu zina nafasi ya kusajili kuongeza nguvu kwenye vikosi vyao dirisha dogo.”

Bares alisema malengo ya mwisho wa msimu ni kumaliza nafasi tano za juu hivyo ili kufikia hilo ni kujipanga na kuhakikisha hawafanyi makosa ya kudondosha pointi na kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji ili kutumia kila nafasi wanayotengeneza.

“Timu yangu haina upungufu mwingi lakini tunaongeza nguvu ili kuhakikisha inakuwa na wachezaji wawili hadi watatu nafasi moja ili ikitokea mmoja kaumia kunakuwa na mbadala ambaye ana uwezo sawa na anayetoka,” alisema.

Related Posts