Matukio yaliytia doa Mkoa wa Dar es Salaam 2024

Dar es Salaam. Wakati zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuufunga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya 2025, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametaja baadhi ya matukio yaliyoutia doa mkoa huo, yakiwemo yanayodaiwa kuwa ya utekaji.

Hata hivyo, Chalamila amesema katika matukio hayo uchunguzi ulibaini si yote yameripotiwa kama ulivyo uhalisia, akifafanua baadhi hayakuwa ya utekaji, bali yanatengenezwa ili kuzua taharuki.

Pamoja na hayo, Chalamila amekiri kuwa tukio la aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao la kutekwa, kisha siku inayofuata mwili wake ulikutwa maeneo ya Ununio, halikubaliki na vyombo vya dola na kwamba bado wanalifanyia kazi.

Chalamila ameeleza hayo leo Jumatatu, Desemba 23, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu salamu  na heri ya sikukuu za mwisho wa mwaka kwa wananchi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla.

Katika mkutano huo, amezungumzia pia mafanikio yaliyopatikana mwaka 2024, huku akilipongeza Jeshi la Polisi chini ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao ya kuimarisha ulinzi na usalama.

Katika maelezo yake, Chalamila amesema miezi michache iliyopita kumekuwa na taarifa zikizagaa mitandano kwa nyakati tofauti zikieleza Dar es Salaam imekuwa na matukio mengi ya utekaji. Hata hivyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, limekuwa likitoa ufafanuzi kuhusu matukio hayo.

“Yapo matukio yaliyoitoa doa Dar es Salaam, lakini yapo machache ambayo wasio na nia njema na mkoa huu walitumia kama faida ya kuchafua mwenendo wa amani jijini Dar es Salama,” amesema Chalamila.

Ametolea mfano jana Jumapili, Desemba 22, 2024 kuna mtoto alipotea, aliyetafutwa lakini kwenye mitandao ikarushwa taarifa kuwa mtoto huyo ameibwa au ametekwa. Amesema polisi ilifanya kazi kubwa ya kumtafuta na kumpata akiwa ndani ya kisima karibu na madrasa anakosoma.

Tukio jingine ambalo Chalamila amesema ‘limetrend’ (kuvuma) kuhusu mtu mmoja (bila kumtaja jina) ambaye hakuonekana, lakini baadaye mwili wake ulipatikana ukiwa umehifadhiwa mochwari ya  Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala.

“Baadhi ya watu walipaza sauti kwamba ametekwa, lakini ukweli kama ambavyo Muliro, alivyosema mtu huyo alikuwa kwenye chombo chake cha usafiri pikipiki kwa bahati mbaya alipata ajali na hakuwa na vitambulisho.

“Wakati mwili unapelewa Mwananyamala alipelekwa akiwa mtu hatambuliki, sasa ilivyokuja kuripotiwa yupo mochwari Watanzania kadhaa wametafsiri kama miujiza au jambo lisiloeleweka. Wakati wote Serikali imeweka utaratibu wa vitambulisho vya Taifa tujitahidi tuwe navyo ili likitokea tatizo iwe rahisi kutambulika,” ameeleza Chalamila.

Mtu anayemzungumzia Chalamila ni mfanyabiashara Daisle Ulomi aliyepata ajali Desemba 11, 2024 saa saba mchana maeneo ya Gereji Mabibo na mwili wake ulitambuliwa na famili yake Desemba 16 katika Hospitali ya Mwananyamala.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi kadhaa waandamizi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Chalamila amesema tukio jingine la Vincent Massawe, anayeishi Kigamboni ambaye kwa muda mfupi ilisemekana ametekwa, lakini baadaye ilibainika alijificha kutokana na madeni yanayomkabili.

“Huu uongo alioufanya Vicent ulichukuliwa kwa taharuki kubwa kwamba Dar es Salaam kuna utekaji mkubwa, jambo ambalo si la kweli,” amesema Chalamila.

Massawe aliyepotea Novemba 18, 2024 baada ya harusi yake, alipatikana Desemba 15, 2024 akiwa amejificha kwa mganga kienyeji wilayani Chakechake, Pemba.

Mbali na hilo, Chalamila amesema tukio jingine lililotia doa ni la Deogratius Tarimo, mfanyabiashara aliyeonyesha anataka kuchukuliwa na baadhi ya mabaunsa maeneo ya Kiluvya.

“Ni kweli wale watu walikuwa wanakusudia kumbeba na pengine wangeweza kwenda kumfanyia vitu vingine siyo sawa. Jeshi la polisi lilifanya kazi kubwa ya kuwatafuta wahusika na kuwakamata nje ya Dar es Salaam,” amesema Chalamila.

Tukio hilo lilitokea Novemba 11, 2024 eneo la Kiluvya na Polisi lilitangaza kuwashikilia watu wanne kutokana na suala hilo.

Mbali na hilo, Chalamila amesema tukio jingine ni lile linalomhusisha Abdul Nondo (Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo), lililotokea stendi ya mabasi ya Magufuli Mbezi Louis.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT- Wazalendo Abdul Nondo akiwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kutokana na kuumizwa kwa kipigo na watu wanaodaiwa kumteka.

Chalamila amesema katika tukio hilo, polisi walihusishwa kuhusika kwa sababu ya kukutwa kwa pingu. Hata hivyo, mkuu wa mkoa huyo amefafanua kuwa neno pingu linavyoonekana wengi wanatafsiri ni polisi.

“Naomba niwaeleze wapo baadhi ya watu wanaweza kuwa na pingu, nguo za polisi au bunduki, lakini sio polisi, wanajeshi au uhamiaji. Kwa kuwa Watanzania wameshafahamu kwamba pingu ina uhusiano na polisi, basi hata majambazi na watu wasiokuwa na nia njema wanaweza kuitumia kuonyesha waliofanya ni polisi,” amesema.

Kutokana na hilo, Chalamila amefanya kikao na polisi ili wanapotekeleza majukumu yao ya ukamataji wavae sare za jeshi hilo, jambo litakaloondoa taharuki kwa Watanzania.

Nondo alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana alfajiri Desemba mosi, 2024 akiwa stendi ya Magufuli akitokea mkoani Kigoma. Hata hivyo, saa tano usiku mwanasiasa huyo alitelekezwa maeneo ya ufukwe wa Coco kabla ya kusaidiwa na wasamaria wema waliompeleka hadi makao makuu ya ACT Wazalendo, Magomeni.

Pamoja na mambo mengine, Chalamila amekiri  tukio la Kibao ni la kihalifu na hakuna mtu atakayeungana na wahalifu katika jambo hilo ambalo lilileta hisia kubwa jamii.

“Hata hivyo, vyombo vyetu vya dola vipo makini kuhakikisha wanapata mnyororo wa watu waliofanya tukio lile. Naamini Jeshi la Polisi likikamilisha taratibu za kiuchunguzi, ikiwemo kuwabaini wahusika watatoa taarifa.

“Watu wengi wanapokuta kuna kuchelewa kutoa taarifa, wanadhani kuna mikakati ya kuficha taarifa. Yapo mambo mepesi unayoweza kutoa taarifa kwa haraka, lakini kuna yale yanayohitaji uchunguzi wa kina ili kuwafikia kwenye mnyororo,” amesema Chalamila.

Kibao, aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya Chadema alikamatwa saa moja jioni Septemba 6, 2024 Tegeta mbele ya Jengo la Kibo Complex, akitolewa kwenye basi alilopanda akielekea mkoani Tanga.

Mwili wa Kibao uliripotiwa kupatikana maeneo ya Ununio, akiwa ameuawa, huku uso wake ukiwa umeharibika kiasi cha kutotambulika.

Kutokana na tukio hilo, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa salamu za pole kwa familia, ndugu, marafiki wa Kibao, huku akiagiza vyombo kufanya uchunguzi na kumpelekea taarifa ya kina kuhusu tukio hilo, akisema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia kila raia ana haki ya kuishi.

Related Posts