Mjamzito, wanawe walivyochinjwa kisa deni la mahindi, muuaji kunyongwa

Sumbawanga. Siku zote wanasema damu isiyo na hatia haiachi kulia, hivi ndivyo unaweza kuelezea tukio lililofanywa na Philipo Mvazi la kumuua mama mwenye ujauzito wa miezi saba na wanawe wadogo wawili kisha naye kujaribu kujiua.

Kama maandiko ya Biblia yasemavyo, anayeua kwa upanga naye atakufa kwa upanga, Jaji Deo Nangela wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga, amemhukumu muuaji huyo adhabu ya kifo, huku akinukuu maneno kuwa uovu kamwe hauwezi kuleta furaha.

Hukumu hiyo imetolewa Desemba 19, 2024 na nakala yake kupatikana katika mtandao wa Mahakama Desemba 23,2024.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Januari 2022 katika eneo la Katumba katika kitongoji cha Dalinyi katika Manispaa ya Sumbawanga ambapo Philipo aliwachinja Judith Rupia aliyekuwa mjamzito na wanawe Godfrey Zumba na William Zumba.

Miili ya watatu hao ikiwa imechinjwa kuanzia kwenye koromeo, iligunduliwa siku kadhaa baadaye ikiwa ndani ya chumba cha kulala na hii ni baada ya rafiki wa Judith, Salome Chrispin na mume wa Judith kubaini simu ya Judith haipatikani.

Salome aliyekuwa shahidi wa kwanza wa Jamhuri, aliieleza mahakama kuwa Januari 14, 2022, rafiki yake alimweleza kuwa anakwenda Utengule kwa huduma ya kidini iliyokuwa inafanyika siku inayofuata na angerejea siku ya Jumapili.

Hata hivyo, siku hiyo jioni, alimtafuta marehemu Judith kwa simu lakini ilikuwa haipatikani, ndipo akaamua kwenda nyumbani kwake na kukuta mlango umefungwa kwa kufuli kwa nje, siku iliyofuata napo alienda na kukuta hali hiyo.

Hali hiyo ilimtia shaka hivyo akaamua kumpigia simu mume wa Judith aitwaye Godfrey Zumba aliyekuwa shahidi wa 4 ambaye alikuwa safarini jijini Dar es Salaam, ambaye naye akamwambia anamtafuta kwa simu mkewe hampati.

Mume wa marehemu akamwambia asubiri awasiliane na wazazi wa Judith kufahamu kama atakuwa amekwenda huko, lakini nao wakathibitisha kuwa mtoto wao hakuwa amekwenda huko na ndipo alimtuma ndugu yake kufuatilia.

Ndugu huyo, Paul Kayanda ambaye ni shahidi wa pili, alifika na wakaenda pamoja hadi nyumbani kwa Judith kwa lengo la kuvunja mlango ili kuangalia kulikoni, lakini kabla ya kwenda, walimchukua mwenyekiti wa kitongoji, Albert Kampamba.

Wakiwa hapo, walivunja kufuli na kuingia ndani ambapo ndani ya chumba cha kulala walikuta mwili wa Judith ukiwa sakafuni pembeni kukiwa na mwili wa watoto wake ambao wote walichinjwa kuanzia kwenye koromeo kwenda nyuma.

Namna mshukiwa alivyobainika

Akinukuu Biblia katika Mithali 21:7 inayosema “Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; kwa sababu wamekataa kutenda hukumu”, Jaji alisema mawimbi yanayovuma yalianza kuvuma kuelekea nyumba ya mzee Vincent Mavazi.

Mzee Mavazi, baba mzazi wa mshitakiwa na aliyekuwa shahidi wa sita, aliieleza mahakama kuwa kwenye Januari 2022, akiwa anahudumia bustani yake, mke wake alimwita kwa sauti akimtaka afike mara moja kwenye chumba cha Philipo.

Alipoitikia wito wa mkewe na kufika katika chumba cha mtoto wao, alikumta mwanawe huyo akiwa katika hali mbaya ya kiasi kwamba hakuwa anaweza kuongea kwa kuwa alikuwa ametapika kila mahali na hata kuchafua nguo zake.

Kwa kushirikiana na mwenyekiti wa kitongoji na jirani, walimwahisha hospitali kwa ajili ya matibabu ambapo daktari aliwaambia kuwa Philipo alikuwa amekunywa sumu, alitibiwa na baadaye aliruhusiwa kurudi nyumbani chini ya uangalizi.

Siku moja, shahidi huyo alisema alipigiwa simu Bernard Kipeta na aliyemwita nyumbani kwa Judith na alipofika alikuta umati wa watu na alifanikiwa kuingia ndani ambapo alikuta mwili wa Judith na wanawe katikati ya dimbwi la damu.

Simulizi ya mzee huyo kwa mujibu wa Jaji Nangela, inaoana na ya shahidi wa saba, Inspekta Msaidizi, Mrisho Mninga ambaye alieleza kuwa Januari 21,2022 akiwa likizo hapo Katumba, alipata taarifa ya mauaji ya kikatili ya Judith na wanawe.

Baada ya kushauriana na wazee wa eneo hilo akiwemo mzee Mavazi, baadaye alijulishwa kuwa mshukiwa mkuu wa mauaji hayo anaweza kuwa Philipo.

Shahidi huyo alieleza kuwa alipata wasaa wa kuzungumza na Philipo ambaye alimthibitishia kuwa yeye ndio mhusika wa mauaji yale na alifanya hivyo,  kwa vile alimpa marehemu mifuko mitatu ya mahindi na mmoja wa maharagwe na hakulipa.

Alieleza kuwa Philipo alimweleza kuwa Judith alikuwa amemlipa pesa kiasi na alipokwenda kudai pesa iliyokuwa imebaki, alikataa kumlipa, jambo ambalo liliamsha hasira yake na kuamua kumuua Judith pamoja na wanawe wawili.

Kulingana na shahidi huyo, Philipo alimwambia kuwa baada ya kufanya mauaji hayo, alirudi nyumbani lakini hakupata usingizi hivyo akaamua kunywa sumu ili kujiua lakini sumu haikuwa kali hivyo alipelekwa hospitali na kupona.

Baada ya kumweleza hivyo, alimtaka asubiri nyumbani hadi polisi waje ambapo alikamatwa na polisi walimtaka waonyeshe nguo alizokuwa amevaa wakati akifanya mauaji hayo na wakamtaka aonyeshe mahali ilipo simu ya Judith.

Aliwaeleza polisi kuwa alikuwa ameitumbukiza chooni lakini polisi kwa kushirikiana na mwenyekiti wa kitongoji na mtendaji wa kata lakini walikwenda kuitafuta simu katika choo hicho na kufanikiwa kupata simu hiyo.

Baada ya kukamatwa na kuandika maelezo yake ya onyo polisi na kukiri kufanya mauaji hayo, alipelekwa kwa mlinzi wa amani, Patrick Lipiki ambaye ni hakimu na alikuwa shahidi wa nane, ambapo aliandika maelezo ya ungamo kukiri kosa hilo.

Mshitakiwa alivyojitetea kortini

Katika ushahidi wake wa utetezi, Philipo alikanusha kabisa kufanya mauaji hayo na kwamba ni afande Mrisho ambaye alikuwa shahidi wa saba ndiye alimshawishi aende kwenye gari lake wazungumze na alimwahidi siku iliyofuata angempeleka mjini.

Alidai yeye alikuwa hafahamu nini kinaendelea na akakanusha kukiri kutenda kosa hilo mbele ya shahidi huyo na kwamba anachokumbuka ni kuwa akiwa mahabusu ya gereza la Sumbawanga, alitakiwa kusaini nyaraka ambazo hazifahamu.

Mshitakiwa alieleza kuwa hafahamu chochote lakini alikiri kuwa hakulazimishwa na mtu yeyote kuandika maelezo yake polisi na kwa mlinzi wa amani,  na kwamba hakufahamu alikuwa mbele ya mlinzi wa amani wala kuandika maelezo ya onyo.

Hukumu ya kifo ilivyotolewa

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande mbili, Jaji alisema ni wajibu wa mahakama kujibu maswali mawili, ambayo ni kama Judith na wanawe walikuwa kifo kisicho cha asili na kama kifo chao si cha asili nani alikisababisha.

Jaji alisema katika kujibu swali la kwanza, hakuna ubishi kuwa Judith na wanawe wawili ni marehemu kwa sasa na kwamba kifo chao hakikuwa cha asili, kwani waliuawa kikatili nyumbani kwao na hilo limethibitishwa na mashahidi.

“Swali linalobaki ni nani aliwaua? Kwa sababu mshitakiwa anakana kabisa kuhusika. Lakini ni ushahidi pekee ndio unaweza kumtoa au kumtia hatiani. Katika kesi hii hakuna shahidi hata mmoja aliyeshuhudia mauaji haya,”alisema Jaji.

Hata hivyo, Jaji alisema ushahidi wa mazingira unaweza kumtia mtu hatiani, na kwa kutizama ushahidi wa mashahidi waliotoa ushahidi wao akiwemo baba mzazi, wote unamlenga mshitakiwa kuwa ndiye aliyetenda mauaji hayo ya kikatili.

“Kuna swali la kujiuliza, kwanini mshitakiwa aamue kunywa sumu? Uhusiano wa kunywa sumu na kufanya mauaji hayo upo kwenye ushahidi wa shahidi wa saba na 10 na unapatikana katika maelezo yake ya ungamo kwa mlinzi wa amani,”alisema Jaji.

“Kuna muunganiko kati ya maelezo hayo ya ungamo na kile walichokisema mashahidi pamoja na vielelezo vilivyopokelewa na mahakama kama ushahidi,  maelezo hayo yalitolewa kwa hiyari na yanaeleza kila alichofanya.”

“Kutokana na uchambuzi wa ushahidi huo uliotolewa mahakamani hata kama hakuna mtu aliyeshuhudia mshitakiwa akifanya mauaji hayo, na maelezo yake mwenyewe ya ungamo, yanatoa jibu moja tu ni Philipo alifanya mauaji hayo.”

Jaji alisema kwa kuangalia silaha iliyotumika katika mauaji hayo na maeneo ya mwili ambayo aliyashambulia, yanathibitisha uwepo wa nia na dhamira ovu ya kuhakikisha kuwa watu hao watatu wanakufa kwa namna alivyowachinja.

Jaji alisema katika kesi ya mauaji, pale inapothibitishwa mshitakiwa ndiye aliyetenda kosa la mauaji ya kukusudia, adhabu ya kosa hilo huwa ni moja tu nayo ni kunyongwa hadi kufa hivyo alimhukumu Philipo Mavazi adhabu ya kifo.

Related Posts