KOCHA wa Tabora United, Anicet Kiazayidi amesema kikosi hicho kiko katika mwelekeo mzuri ingawa ana kazi kubwa ya kufanya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kutokana na ushindani mkubwa uliopo.
Kauli ya kocha huyo inajiri baada ya timu hiyo kumaliza michezo yake ya raundi ya kwanza ikiwa nafasi ya tano na pointi 25, huku ikonyesha ushindani mkubwa kwa vigogo wa soka nchini, kufuatia kuzifunga Yanga mabao 3-1 kisha Azam FC mabao 2-1.
“Tuko katika mwelekeo mzuri lakini tuna kazi kubwa ya kufanya mzunguko wa pili ili kuendana na ushindani, naamini kwa kikosi kilichopo na maboresho tutakayoyafanya tutaweza kutimiza malengo yetu ya kushikilia tulipo au kusogea juu zaidi,” alisema.
Kocha huyo aliongeza kuwa jambo nzuri kwa sasa hawana mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara, hivyo inampa nafasi ya kuendelea kukisuka vyema kikosi hicho kwa michezo ijayo, huku akijivunia morali na ushirikiano anaoupata kutoka kwa wachezaji.
Anicet aliyezifundisha timu za AS Vita Club, FC Simba Kolwezi, FC Les Aigles du Congo na Maniema Union zote za DR Congo, tangu ajiunge na kikosi hicho Novemba 2, mwaka huu akichukua nafasi ya Mkenya Francis Kimanzi, hajawahi kupoteza mchezo wa Ligi Kuu Bara akishinda michezo minne na kutoka sare miwili.
Katika michezo hiyo, Tabora ilizifunga Mashujaa FC (1-0), Yanga (3-1), KMC (2-0), Azam (2-1), huku sare pekee zikiwa na Singida Black Stars (2-2) na Coastal Union (1-1).
Sare ya bao 1-1 iliyoipata Tabora dhidi ya Coastal Union Desemba 17 mwaka huu iliifanya timu hiyo kufikisha michezo saba mfululizo bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 4-2 na JKT Tanzania Oktoba 18.