Arumeru. Mmoja wa ndugu wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu ofisi ya Msajili wa Hazina, Amos Nnko, Obilio Mbise, amesimulia kauli ya mwisho ya marehemu saa chache kabla ya kupata ajali.
Amos alifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Same, mkoani Kilimanjaro, jana mchana Jumapili, Desemba 22, 2024.Katika ajali hiyo, pia binti yake wa kwanza, Maureen Nnko alifariki.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwa marehemu Kijiji cha Seela, Kata ya Seela Sing’isi wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha leo Jumatatu Desemba 23, 2024, Mbise amesema Jumamosi Desemba 21, 2024 Nnko aliwapigia simu kuwajulisha kuwa anaenda na familia kwa ajili ya kusherehekea sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.
“Amos alinipigia simu Desemba 21, 2024 kwamba atakuja Arusha kwa ajili ya kula sikukuu pamoja na sisi na tarehe 22, asubuhi alitoka Dar es Salaam, ilipofika saa sita mchana, tuliwasiliana naye tena, akatuambia amefika Bwiko, ila baada ya hapo hatukuwasiliana naye tena,” amesimulia ndugu huyo.
Hata hivyo, amesema muda mchache baadaye alipigiwa simu na mtu aliyemtaja kwa jina la Paulo Sarakikya akimjulisha kwamba ndugu yao amepata ajali eneo la Same na majeruhi kwa wakati huo walikuwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Same.
Mbise amesema baada ya kupata taarifa hizo, aliongozana na baadhi ya ndugu kuelekea Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi walikoambiwa baadhi ya majeruhi wanahamishiwa hapo na wengine walipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.
Ndani ya gari hilo, Nnko alikuwa na abiria watano, wanne ni majeruhi akiwamo mkewe na wanawe wawili na mwanafamilia mmoja, huku yeye na binti yake wakifia eneo la ajali.
Akizungumzia utaratibu wa maziko, amesema kwa sasa wanasubiri mke wa marehemu, Agnes Nnko apate nafuu ili waweze kushirikiana naye na Ofisi ya Hazina kupanga taratibu za maziko.
“Kuhusu taratibu za maziko tunasubiri mke wa marehemu atoke KCMC ili tupange pamoja na yeye, tuliwasiliana na ofisini kwake akatuambia ametuma watu tupange nao pia taratibu za maziko,”amesema Mbise.
Amesema kwa sasa baadhi ya ndugu na watumishi wengine kutoka ofisi ya Hazina, wameelekea wilayani Same kuchukua miili ya marehemu ili kuileta katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mt Meru.
“Tunaendelea kusubiri na walioenda Same wakirudi tutaendelea na vikao kwa ajili ya kupanga namna ya kufanya maziko. Amos kwenye familia alikuwa mtu mwema kabisa, anapenda familia yake ni mtu alikuwa napenda dini, huo ni ukweli alikuwa anashirikiana na majirani na sijawahi kuona akiwa na ugomvi na mtu yoyote,”amesema.
Awali kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu ilieleza kuwa Nnko alikuwa na mkewe, pamoja na watoto wengine Marilyn, Melvin na mwanafamilia mwingine, Saylvana ambao wanaendelea kupatiwa matibabu KCMC na Mawenzi.
“Mipango ya mazishi inaendelea kuratibiwa na familia ya marehemu kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina,”imeeleza taarifa hiyo.