Dar es Salaam. Wanandoa, Shabani Adamu na mkewe Husna Issa pamoja na mtoto wao, Mussa Shabani wanaokabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine, wanakusudia kumuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) wakiomba kukiri makosa na kupunguziwa adhabu.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la kusafirisha gramu 41.49 za dawa za kulevya aina ya heroine.
Wakili wa mshtakiwa huyo, Nehemia Nkonko ametoa maelezo hayo leo Jumatatu, Desemba 23, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi hiyo ilipotajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Nkonko ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini amesema, “Mheshimiwa hakimu, wateja wangu wanakusudia kuandika barua ya kufanya majadiliano na DPP ya kukiri shtaka lao na kuimaliza kesi yao.”
Nkonko baada ya kutoa taarifa hiyo, Serikali imesema bado haijapata barua hiyo, hivyo wakiipata wataifanyia kazi.
“Mheshiwa hakimu, barua hiyo ikitufikia tutaifanyia kazi,” amedai Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele.
Awali, Mwakamele alidai kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza usikilizwaji, baada ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo, wiki iliyopita.
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili ameahirisha kesi hadi Januari 6, 2025 itakapoanza kusikilizwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kwa kuwa shtaka linalowakabili halina dhamana na pia idadi ya dawa wanazodaiwa kusafirisha zimevuka uzito wa gramu 20.
Kwa mujibu wa sheria, dawa za kulevya aina heroine, cocaine na nyingine zinapozidi gramu 20 na kuendelea, washtakiwa hawezi kupata dhamana, lakini zikiwa chini ya hapo wanaweza kupata dhamana.
Itakumbukwa Desemba 11, 2024 washtakiwa hao walisomewa hoja za awali mahakamani hapo.
Mahakama hiyo ilielezwa namna washtakiwa walivyodakwa na kiasi hicho cha dawa nyumbani kwao Manzese, jijini Dar es Salaam.
Katika maelezo hayo ilielezwa kuwa Julai 11, 2024, Koplo Jackson alipata taarifa kwamba eneo la Manzese Kilimani kuna watu wanajihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Baada ya kupata taarifa hizo, Koplo Jackson akiwa na wenzake waliweka mtego wakitaka kuuziwa dawa hizo. Walikwenda eneo hilo wakiwa na mjumbe na wakawakamata washtakiwa na kufanya upekuzi katika nyumba yao.
“Katika upekuzi huo walikamata vitu mbalimbalim ikiwemo mfuko wa nailoni angavu wenye unga wa chengachenga, mifuko miwili ya nailoni yanye unga mweupe unaosadikika kuwa ni dawa za kulevya, kitambulisho cha Nida cha Adam, simu tatu, fedha taslimu Sh130,000, kisu, kijiko cha chakula na jiko la gesi,” alidai Thomas wakati akisomea hoja za awali.
Alidai baada ya upekuzi, hati ya kukamata mali ilijazwa na kusainiwa na washtakiwa Adamu, Husna, askari na mjumbe isipokuwa Musa.
Hata hivyo, unga huo ulichunguzwa katika Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kubainika ni dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa gramu 41.49.
Washtakiwa walipohojiwa polisi walikiri kutenda kosa hilo. Baada ya kusomwa hoja hizo, washtakiwa walikana kutenda kosa hilo isipokuwa majina na anwani zao, kukamatwa, kufikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka.