Tasaf yapeleka neema Upenja | Mwananchi

Dar es Salaam. Wananchi wa Upenja na Shehia za jirani, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Ungujja, sasa wataondokana na adha ya kufuata huduma za afya mbali baada ya kuzinduliwa kwa kituo cha afya.

Kituo hicho kitakachokuwa kikitoa huduma mbalimbali, ikiwemo za kibingwa kimezinduliwa ikiwa ni utangulizi kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kituo hicho kilichopo Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kazkazini Unguja, Visiwani Zanzibar kimejengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), kimegharimu zaidi ya Sh342 milioni.

Akizungumza jana Jumapili, Desemba 22, 2024, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi wa Zanzibar, Rahma Kassim Ali amesema kufunguliwa kwa kituo hicho kutachangia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya muda wote kwa wakazi wa Upenja na shehia za karibu.

Amesema Tasaf imekuwa na mchango mkubwa katika kuinua hali za maisha na kipato kwa jamii nzima kupitia utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini, huku akiwasihi wananchi  wa shehia ya Upenja kutunza miundombinu uliyojengwa  ili idumu kwa muda mrefu na kunufaisha  wananchi wengi.

“Tunaishukuru na kuipongeza Tasaf kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo huu wa kituo cha afya Upenja. Kituo hiki ni muhimu, kwani kitasaidia upatikanaji wa huduma zote muhimu za afya kama vile upasuaji, huduma za kinywa na meno,  mama na mtoto, huduma ya wagonjwa wa nje na huduma ya mionzi,” amesema.

Akizungumza mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, ambaye ni Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano wa Tasaf, Japeht Boaz amesema jumla ya Sh15.18 bilioni zimetumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali visiwani Zanzibar.

Kati ya hizo, zaidi ya Sh1.9 bilioni zilitumika kununua vifaa vya utekelezaji na Sh13 bilioni zilitumika kulipa ujira kwa kaya za walengwa zaidi ya 35,000.

“Miradi iliyotekelezwa ni katika sekta ya afya, maji, elimu mazingira misitu, barabara, uvuvi, kilimo umwagiliaji na miundombinu,” amesema.

Akizungumzia utekelezaji wa kipindi cha Pili, Tasaf amesema zilitolewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi 15 ya kuendeleza miundombinu katika sekta ya elimu, afya na maji, ambayo imegharimu zaidi ya Sh3.1 bilioni.

“Kwa mwaka huu 2024, miradi mitatu yenye thamani ya Sh750 milioni imetekelezwa na kukamilika kwa upande wa Unguja katika shehia za Bambi, Kizimkazi dimbani na Upenja. Miradi mingine inaendelea kutekelezwa katika shehia za Donge, Uzi na Kizimkazi dimbani kwa jumla ya Sh306.6 milioni,” amesema.

Kukamilika kwa miradi hiyo kwa mujibu wake kutaongeza wigo wa upatikanaji wa huduma muhimu katika maeneo husika na kuchochea maendeleo ya kijamii na kuichumi na hatimaye kuendelea kutokomeza umaskini wa kaya.

Related Posts