Rombo. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema iwapo Watanzania wangekuwa na ari ya kujituma kama wanavyofanya Wachaga, nchi ingekuwa mbali kwa maendeleo.
Kikwete ametoa sifa hizo kwa Wachaga, huku akiyahusisha baadhi ya makundi ya watu nchini, ambayo hata kulima kwa ajili ya mlo wao wanalazimika kusukumwa.
Kikwete ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Desemba 23, 2024 alipowaongoza maelfu ya wanariadha katika mbio za Rombo Marathon zilizofanyika katika Hifadhi ya Msitu wa Rongai wilayani Rombo, Kilimanjaro.
“Kuna maeneo hapa nchini watu hata kujilimia chakula chao inabidi usukumane nao, lakini hakuna Mchaga utakayemsukuma kwa kujiletea maendeleo, na hiyo ndio siri, uzuri Wachaga hawasahau kwao kila mwaka wanakwenda kuhesabiwa,” amesema.
Kwa mujibu wa Kikwete, mtindo wa kwenda nyumbani kila mwisho wa mwaka unajenga ushawishi kwa wengine kuonyesha hatua za maendeleo walizopiga.
“Niwapongeze wananchi wa Rombo kwa moyo wenu wa kujituma na kujiletea maendeleo, mimi nimefanya kazi wilayani, mkoani, wizarani na katika ngazi ya juu kabisa ya uongozi wa nchi yetu, Watanzania wote wangekuwa na ari ya wachaga nchi yetu ingepiga hatua kubwa, endeleeni na moyo huo,” amesema.
Pamoja na hayo, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuiunga mkono Serikali ili iendelee na juhudi za kuleta maendeleo.
Ametumia jukwaa hilo pia kumpongeza mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda kwa kile alichosema anajituma.
Akizungumza katika tukio hilo, Profesa Mkenda ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema fedha zitakazopatikana katika mbio hizo zitatumika kuboresha vyoo vya shule za msingi, sekondari na upanuzi wa Hospitali ya Huruma wilayani humo.
“Kile kitakachopatikana cha ziada kitatumika kuchangia upanuzi wa Hospitali ya Huruma ili kuongeza nguvu na kuifanya iwe Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,” amesema.
Anna Ulirka, mmoja wa walioshiriki mbio hizo, amesema mbali na riadha, tukio hilo limewakutanisha wakazi wa Rombo na kubadilishana mawazo.
“Tumefarijika sana kwa mbio hizi za Marathon, kwani zimetukutanisha na ndugu, jamaa na marafiki ambao kwa mwaka mzima tulikuwa hatujaonana. Tunaomba marathon hii iwepo kila mwaka,” amesema.