Shinyanga. Ujenzi wa kiwanja cha ndege Ibadakuli katika Manispaa ya Shinyanga umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2025.
Mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania na kutekelezwa na Mkandarasi China Hennan International Corporation Group Co. Ltd (CHICO) utagharimu Sh49.18 bilioni.
Msimamizi wa Tanroads Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Chiyando Matoke amesema sehemu kubwa iliyobaki ni ujenzi wa jengo la abiria, huku barabara ya kuruka na kutua ndege ikiwa tayari imekamilika.
“Uwanja wa ndege Ibadakuli umeanza kufanyiwa ukarabati pamoja na upanuzi wa uwanja huo baada ya kukaa muda mrefu bila kufanya kazi na kusababisha wananchi wanaohitaji kutumia usafiri wa anga kwenda Mwanza,” amesema Matoke
Kwa mujibu wa Mhandisi wa Ujenzi, Ruburi Kahatano, mradi huo ni wa kimkakati na utaimarisha usafiri wa anga, usafirishaji wa mizigo na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru, ameeleza kuwa kukamilika kwa kiwanja hicho kutaleta fursa mpya za kiuchumi kwa wakazi wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla.
Kakuru amesema uboreshaji wa miundombinu ya usafiri, ikiwemo kiwanja cha ndege Shinyanga, utaleta manufaa makubwa kwa wakazi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
“Kwa sasa, ndege zimeanza kutua kwa dharura wakati wa mchana, ishara kwamba maendeleo ya ujenzi yanaendelea vizuri,” amesema.