Amorim apewa rungu ishu tata ya Rashford Man United

BILIONEA Sir Jim Ratcliffe na bodi ya Manchester United hawataingilia uamuzi wa kocha Ruben Amorim juu ya mchezaji Marcus Rashford.

Staa huyo wa kimataifa wa England amewekwa nje ya kikosi cha Man United kwa mara ya tatu mfululizo ndani ya siku nane, wakati kikosi hicho kilipokumbana na kipigo kutoka kwa Bournemouth kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika uwanjani Old Trafford, juzi Jumapili.

Jambo hilo limezidi kuchochea uwezekano wa Rashford, 27, kuondoka kwenye kikosi hicho wakati dirisha la usajili wa Januari litakapofunguliwa wiki ijayo, huku beki wa kulia na nahodha wa zamani wa kikosi hicho, Gary Neville, akisema huenda staa huyo atakuwa ameshacheza mechi yake ya mwisho kwenye kikosi hicho na kwamba hataonekana tena akiwa na miamba hiyo ya Old Trafford.

Rashford mwenyewe alikiri siku moja baada ya kuweka nje kwenye Manchester derby, Jumapili iliyopita, kwamba hatima ya maisha yake ipo kwingineko.

Lakini, kwa kila mechi ya Man United ambayo itacheza bila ya huduma ya Rashford inaweza kuiweka timu hiyo kwenye nafasi nzuri ya kupata pesa kwenye dirisha la Januari kama itaamua kumpiga bei jumla.

Man United imeweka wazi milango ya kuachana na Rashford kwa mkopo, lakini kuhusu pesa itahitaji walau ivune Pauni 40 milioni kwenye mauzo yake.

Awali, mmiliki mpya wa Man United, bilionea Ratcliffe alihitaji sana kupata huduma bora kutoka kwa Rashford baada ya kufunga mabao 30 kwenye kikosi hicho misimu miwili iliyopita. Hata hivyo, kwa sasa tajiri huyo hana presha na wala wakurugenzi wake hawana wasiwasi juu ya kumpoteza Rashford, akiwamo mkurugenzi mtendaji mkuu mpya, Omar Berrada.

Kocha Amorim alisema tena kwa msisitizo tangu alipoanza kumuondoa Rashford kwenye kikosi chake wikiendi iliyopita kwamba huo ni uamuzi wake binafsi na aliendelea kusisitiza hilo kwenye mechi ya kipigo dhidi ya Bournemouth.

Amorim alisema: “Ni uamuzi wangu na siku zote utabaki kuwa hivyo. Ni suala la uteuzi tu wa kikosi. Nataka kuona ubora kutoka kwa wachezaji wangu, hivyo tutajaribu mambo tofauti kwa wachezaji tofauti. Huo ndio mpango wangu.”

Kwenye mchezo wa Man City, Rashford na Alejandro Garnacho waliwekwa benchi, lakini winga huyo wa Kiargentina alirudishwa kwenye kikosi akianzia benchi dhidi ya Tottenham Hotspur na Bournemouth. Rashford anaripotiwa kwamba hakufanya mazoezi na wenzake baada ya mechi ya Man City, akidai kwamba anaumwa na hakusafiri na timu hiyo kwenye mechi zake za ugenini Etihad na Tottenham.

Alionekana Old Trafford juzi Jumapili, akiwa kwenye tracksuit ya klabu hiyo, na mechi ijayo ya Boxing Day dhidi ya Wolves itasubiriwa kwa hamu kuona kama atakuwa na nafasi ya kurejea kwenye kikosi hicho cha Amorim.

Kocha huyo mpya wa Man United amekuwa akifanya mabadiliko mengi sana ya wachezaji kwenye kikosi chake akijaribu kutafuta wale watakaoendana na staili yake ya uchezaji ya 3-4-3. Kwenye hilo la kuhusu wachezaji watakaocheza uwanjani Molineux, kocha Amorim alisema: “Inategemea. Ngoja tuone.”

Related Posts