Agosti 19, 2024 ni moja kati ya siku ya kukumbukwa katika mwaka huu, kwani liliibuka tukio kubwa la binti wa Kitanzania kufanyiwa unyanyasaji wa kingono.
Binti huyo alibakwa na kundi la wanaume na kipindi unyama huo unafanyika, vijana hao walikuwa wakirekodi kile wanachokifanya kisha baada kuvujisha.
Baada ya video hizo kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, Watanzania, walianza kupaza sauti za kulaani vikali kitendo hicho.
Walishinikiza mamlaka za kiusalama kuwatia nguvuni vijana hao kisha kuwafikisha katika chombo cha sheria yaani mahakamani, ili waweze kushikishwa adabu kwa kile walichokifanya.
Kutokana na nchi yetu kuheshimu na kuzingatia utawala sheria ikiwemo sheria na haki za binadamu, Agosti 19, 2024 vijana hao walitiwa nguvuni na Jeshi la Polisi kisha kupelekwa mahakamani. Ilisadikika vijana hao walitekeleza unyama kwa amri ya mkuu wao wa kazi waliyemwita kwa jina la ‘Afande’
Baada ya ushahidi kukamilika, ndipo Septemba 30, 2024 vijana hao walikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa uhalifu wa kinyama walioufanya.
Tukirejea tena Agosti 19, 2024 mbali na kuibuka kwa tukio lililodokezwa kupitia aya tangulizi, ila tarehe hiyohiyo kuljitokeza tukio lingine ambalo liliteka hisia kubwa katika jamii.
Mwandishi wa habari kutoka gazeti la “Mwananchi” alifanya mawasiliano na aliyekuwa Kamanda wa Polisi – Mkoa wa Dodoma kwa wakati huo, SACP Theopista Mallya.
Wakati akijibu maswali ya mwandishi wa habari, alidai kuwa mbali na kufanyika tukio ambalo ni uvunjaji wa sheria, lakini mwathirika wa tukio (binti aliyebakwa), naye alikuwa akifanya biashara ya ngono.
Baada ya kutolewa kauli hiyo watu wengi hawakupendezwa nayo, kwani ilionekana kuwa na mrengo wa kiunyanyasaji.
Tarehe hiyohiyo, msemaji wa jeshi, David Msime alitoa tamko la kutounga mkono kauli iliyotolewa RPC-Dodoma na kusema haikuwa msimamo wa Jeshi la Polisi.
Kamanda huyu hakudumu ofisini na hii nahusianisha na matukio kadhaa ya watendaji waliojikuta wakipoteza nyadhifa zao baada ya kutoa kauli zenye utata kwa jamii.
Kwa mtazamo wangu, kuna elimu ambayo inatakiwa kufundishwa kwa watumishi wote. Naamini elimu hiyo itaondoa tatizo ambalo kama hatutakuwa makini litakuwa ni tatizo ‘sugu’.
Ili kutibu changamoto hiyo, ninapendekeza elimu ya mawasiliano kwa umma ifundishwe kwa watumishi wote.
Mawasiliano kwa umma ni taaluma inayohusu uwasilishaji wa taarifa, elimu, na habari katika hadhira pana kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo vyombo vya habari.
Taaluma hii inachunguza jinsi ujumbe unavyoundwa, unavyosambazwa na unavyopokelewa na hadhira lengwa.
Taaluma hii inatoa stadi na mbinu kwa mwasilishaji wa ujumbe kujua nini cha kusema, wapi, na kwa wakati gani kwa niaba ya chombo au taasisi anayotoka mhusika.
Kupitia taaluma ya mawasiliano kwa umma, mtumishi anapata mbinu na stadi za kutoa taarifa kwa namna ambayo inalinda na kuboresha sifa ya taasisi anayotoka, wakati huohuo akihakikisha mawasiliano hayo, yanafanywa kwa wakati na mahali sahihi.