Mgunda avimbia ubora wa Amoah

KOCHA wa Namungo, Juma Mgunda, ameonyesha matumaini makubwa na beki mpya wa kati, Daniel Amoah, ambaye alisajiliwa katika dirisha hili la usajili.

Mgunda amesema kuwa Amoah ana uwezo mkubwa na anaweza kuwa chachu ya kuboresha ukuta wa timu yake, ambao hadi sasa umeruhusu mabao 18 katika michezo 15 ya Ligi Kuu Bara.

Akizungumza kuhusu usajili huo, Mgunda alisema anaamini Amoah atasaidia sana katika kuimarisha safu ya ulinzi ya Namungo, hasa kutokana na changamoto walizokutana nazo katika duru la kwanza la ligi.

Alikiri kwamba mojawapo ya maeneo ambayo Namungo inahitaji kuboresha ni ulinzi, huku pia akitaja kuwa safu ya ushambuliaji ya timu hiyo imefunga mabao tisa tu hadi sasa, jambo ambalo linahitaji kurekebishwa.

“Daniel ni beki mzuri, mwenye uzoefu na nguvu,” alisema Mgunda. “Anaijua vizuri ligi hii, na ni mtu ambaye anaweza kuingia haraka kwenye mfumo wangu. Nimekuwa nikimfuatilia kwa muda mrefu, na kwa ufanisi wake akiwa Azam, nina imani atakuwa msaada mkubwa kwetu.”

Amoah, ambaye ni maarufu kwa kutumia nguvu na akili katika kazi yake ya ulinzi, alikuwamo katika kikosi cha Azam kabla ya kupoteza nafasi ya kucheza mbele ya Yeison Fuentes, Yannick Bangala (kabla hajaondoka), na Yoro Mamadou Diaby. Hata hivyo, Mgunda ana imani kuwa nafasi ya Amoah katika timu ya Namungo ni muhimu na itakuwa ni suluhisho kwao.

Related Posts