Kiluvya United bado hakijaeleweka | Mwanaspoti

KICHAPO cha mabao 3-1, ilichokipata Kiluvya United wiki iliyopita dhidi ya Mbuni, imemfanya kocha mkuu wa kikosi hicho, Zulkifri Iddi ‘Mahdi’ kudai sababu kubwa zilizowanyima ushindi ni kutokana na kukosa utulivu wa kumalizia vyema nafasi.

Timu hiyo iliyoshinda mchezo mmoja tu kati ya 13 iliyocheza baada ya kutoka sare pia mmoja na kupoteza 11, ilikumbana na kichapo hicho kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha hivyo, kukifanya kuendelea kusalia mkiani na pointi nne.

“Licha ya kutawala mchezo, ila tulipoteza kwa sababu ya kukosa umakini wa kumalizia nafasi tulizozipata, tuna kazi kubwa sana ya kufanya ili kuhakikisha tunarekebisha changamoto hiyo kwa haraka zaidi kabla ya mambo hayajaendelea kuharibika.”

Kocha huyo aliongeza, bado hakuna balansi nzuri ya kuzuia na kushambulia hivyo anarudi katika uwanja wa mazoezi kufanyia kazi changamoto hiyo, huku akiwaomba mashabiki kuendelea kuwapa sapoti akiamini bado wana nafasi ya kujinasua mkiani.

‘Mahdi’ aliyewahi kufundisha timu mbalimbali zikiwemo za Namungo FC, Cosmopolitan na Singida United amejiunga na kikosi hicho akichukua nafasi ya Twaha Beimbaya aliyeanza nayo msimu kisha kutimuliwa kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo.

Related Posts