Raizin Hafidh kiroho safi Mtibwa

MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh amesema endapo dili lake la kujiunga na Kagera Sugar litakwama dirisha hili, atakichezea kikosi hicho kiroho safi ili kukipambania kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu uliopita.

Akizungumza na Mwanaspoti, Raizin mwenye mabao 10 na kikosi hicho alisema licha ya Kagera Sugar na Pamba kuonyesha nia ya kumhitaji ila anaheshimu sehemu alipo, kwani hataki kuharakisha dili hilo baada ya viongozi kuweka ngumu kuondoka.

“Ni kweli nimekuwa na ofa nyingi lakini sijafanya maamuzi yoyote hadi sasa, viongozi na benchi letu la ufundi wamekuwa nami bega kwa bega wakihitaji niendelee kukipigania kikosi ili kipande Ligi Kuu Bara hivyo, naheshimu sana matakwa yao.”

Raizin ni miongoni mwa nyota wanaofanya vizuri kwa sasa na anahitajika na Kocha wa Kagera Sugar, Mmarekani Melis Medo aliyewahi kufanya naye kazi katika kikosi cha Mtibwa, ingawa viongozi wameonyesha hawako tayari kumuachia kipindi hiki.

Nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Dodoma Jiji huku akizichezea Gwambina na Coastal Union, alisema anawaomba mashabiki waendelee kuwaunga mkono ili kuirejesha Mtibwa Ligi Kuu, kwani bila ya wao hawatofikia malengo hayo.

Related Posts