Rombo. Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili na Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya na Tiba, Profesa Mohamed Janabi, amewasisitiza wakazi wa Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro kunywa maji akisema mandhari ya maeneo ya juu ya mlima husababisha damu kuwa nzito.
Akizungumza na wakazi hao jana Jumatatu Desemba 23, 2024, Profesa Janabi amesema katika maeneo ya juu, kama ilivyo Wilaya ya Rombo, damu za watu huwa nzito zaidi kutokana na mabadiliko ya kimo cha ardhi, hivyo kunywa maji ni muhimu kwa afya zao.
“Hapa Rombo, maji ni muhimu sana kwa sababu mpo juu, mkiwa juu damu inakuwa nzito kidogo, hivyo ni muhimu kunywa maji,” amesema Profesa Janabi.
Pia, amewahimiza kuzingatia ulaji wa matunda na mbogamboga ili kudumisha afya njema na kuongeza nguvu za mwili.
“Matunda na mboga ni muhimu kwa afya na kupumzika pia ni muhimu, hizi zote ni hatua zinazosaidia mwili kuwa na afya nzuri kila wakati,” amesema Profesa Janabi.
Katika mahojiano na Mwananchi Digital, baadhi ya wakazi hao wamesema changamoto zinazowakumba katika kunywa maji, hasa kutokana na hali ya hewa baridi inayokumba wilaya hiyo.
Jenifa Shayo, mmoja wa wakazi wa Rombo, amesema kunywa maji ni jambo la nadra kwao kutokana na baridi kali.
“Sikumbuki ni lini nilikunywa maji, labda wiki moja iliyopita. Hapa kunywa maji ni changamoto kubwa kwa sababu ya baridi,” amesema Jenifa.
Adam Tesha, mkazi wa wilaya hiyo, amesema hali ya hewa ya baridi inafanya maji kuwa vigumu kunyweka.
“Kwa hapa kwetu, hata huwezi kuweka maji kwenye friji kwa sababu hali ya hewa ni baridi sana, kwa hiyo, mazingira hayawezi kumshawishi mtu kunywa maji, kwa kweli ni mtihani,” amesema Tesha.