Spika Maulid ataka tathmini uwekezaji nyumba za biashara

Unguja. Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Maulid amezitaka taasisi zinazohusika na sekta ya utalii kufanya tathmini ya uwekezaji wa nyumba za biashara kwa wageni na kuishauri Serikali juu ya mwelekeo sahihi wa kuimarisha utalii kwa kuzingatia masilahi ya Taifa.

Ametoa kauli hiyo leo Desemba 24, 2024 wakati akizindua Hoteli ya Moyo Mzuri Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 61 ya Mapinduzi.

Spika Maulid amesema baraza litaendelea kutunga sheria nzuri za kulinda rasilimali.

Amesema kuimarika kwa miundombinu ya kiuchumi na kijamii kutaifanya Zanzibar kuwamo kwenye ramani ya dunia na kuwa miongoni mwa maeneo bora kwa uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

 “Uwekezaji wa sekta ya ujenzi wa nyumba za biashara kwa wageni nchini umekuwa ndio uwekezaji wa pili unaoongoza kwa kuleta mitaji mikubwa nchini ikifuatiwa na uwekezaji wa sekta ya hoteli, nitoe wito kufanya tathmini ya utalii na kuishauri Serikali,” amesema Spika Maulid. 

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 37 ya miradi yote ya uwekezaji iliyosajiliwa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji (Zipa) katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane ni miradi ya hoteli ikifuatiwa na asilimia 22 ya miradi ya nyumba za biashara.

“Takwimu hizi zinadhihirisha kuwa taswira ya utalii wetu sasa unabadilika kwa kasi. Wageni wengi wanaokuja nchini wanapendelea kubaki kwa siku nyingi ili kufurahia mandhari nzuri ya visiwa vyetu, ndio maana biashara ya ununuzi na ukodishwaji wa nyumba kwa wageni imezidi kushamiri katika kipindi hiki,” amesema Spika Maulid.

Amewataka wawekezaji na taasisi zote zinazoshughulika na uwekezaji kuendelea kutunza mazingira ya visiwa hivyo kwa masilahi ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

“Tuendelee kutekeleza na kusimamia vyema sheria ya mazingira katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya uwekezaji. Sote kwa pamoja tuwe walinzi wa rasilimali zetu kwa masilahi ya Taifa letu,” amesema. 

Katika kuhakikisha kuwa watalii wanaokuja nchini wanapata hifadhi za malazi zenye mandhari nzuri wanapokuwa mapumzikoni, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeweza kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya hoteli.

Kwa mujibu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale idadi ya watalii wanaoingia nchini imezidi kuongezeka, mwaka 2023, Zanzibar ilipokea watalii 640,000 na inalenga kufikia milioni moja ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi Mtendaji wa Zipa, Saleh Saad Mohamed amesema mpaka sasa mamlaka imesajili miradi 424 ya Dola 5.9 bilioni za Marekani (Sh14.278 trilioni).

“Miradi hii itatoa ajira 22, 000, hii ni kutokana na miongozo tunayopewa inafanyiwa kazi,” amesema Mohamed.

Mwekezaji wa hoteli hiyo, John Mbwambo amesema mradi huo umetumia Dola 1 milioni za Marekani (Sh2.420 bilioni) na unatarajiwa kuajiri wafanyakazi 33, mpaka sasa wameajiriwa wafanyakazi 17 wote ni wazawa.

Related Posts