Karia atoa msimamo ombi la simba, yanga

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesisitiza kuwa ni jambo la busara na hekima kuheshimu katiba inayoziongoza klabu zote nchini zilizopo chini ya mwamvuli wa shirikisho hilo.

Karia ameyasema hayo akijibu hoja iliyotolewa na Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu kisha kuungwa mkono na Rais wa Yanga, Hersi Said ikimtaka aendelee kusalia madarakani kwa kipindi kijacho.

Viongozi hao waliyasema hayo wakiwa kwenye mkutano wa kawaida wa TFF uliofanyika Desemba 21, mwaka huu, Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo hoja yao kubwa ilikuwa ni namna Karia uongozi wake ulivyo na tija kwa timu za Taifa ikiwemo Taifa Stars, timu za vijana na kwa upande wa wanawake kuendelea kufanya vizuri.

Akijibu hoja hiyo alipozungumza katika Mkutano Mkuu wa Coastal Union uliofanyika ulioambatana na uchaguzi mkuu wa klabu hiyo, Karia alisisitiza kuwa ni muumini anayeheshimu na kufuata katiba inayowaongoza huku pendekezo hilo lisichukuliwe kimihemko kwani bado muda wake wa uongozi haujaisha, vinginevyo wasubiri kutangazwa kwa uchaguzi na Mkutano Mkuu ndio utaamua.

“Hivi karibuni kwenye mkutano wetu wa kawaida wa TFF walizungumza na kusikika viongozi wa timu za Simba na Yanga kuhusu mimi kuendelea kuongoza, lakini niseme tu kwamba muda wangu haujafika mwisho na wala uchaguzi haujatangazwa.

“Kama watu wanamtaka Karia wasubiri uchaguzi utakapotangazwa. Lazima katiba tuziheshumu na twende katika utaratibu ambao unakubalika,” alisema Karia ambaye tayari kwa sasa ni rais wa TFF kwa awamu ya pili akibakiwa na mwaka mmoja katika uongozi wake.

Wakati huohuo, mwenyekiti aliyemaliza muda wake ndani ya Coastal Union, Steven Mguto alisema kwa sasa hakuna anayeweza kuvaa viatu vya Karia kuiongoza TFF, hivyo ni vyema kiongozi huyo akaendelea na nafasi hiyo.

“Tunampongeza sana rais wa TFF kwa namna ambavyo analiongoza shirikisho letu. Katika kipindi chake chote kumekuwa na mafanikio makubwa kwa Taifa letu. Timu zetu za Taifa zinaendelea kufanya vizuri. Tumepata bahati ya kuhodhi michuano ya CAF na sisi Coastal Union tunaungana na wenzetu wa klabu za Simba na Yanga kutaka rais wetu aendelee, bado hatujaona ambaye ataweza kumrithi,” alisema Mguto huku hoja yake hiyo ikiungwa mkono na wajumbe zaidi ya 200 waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Klabu ya Coastal Union.

Related Posts