Same. Mawasiliano ya barabara katika eneo la Kizangaze, Kijiji cha Mpirani, Kata ya Maore, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro, yamekatika baada ya kingo za daraja la Kizangaze kusombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.
Kukatika kwa daraja hilo kumesababisha kata nne za Maore, Ndungu, Kihurio na Bendera kukosa mawasiliano. Hali hii imeathiri wasafiri kutoka mikoa mbalimbali waliokuwa wakielekea wilayani humo kwa ajili ya kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Mvua hizo zilizoanza usiku wa Desemba 20, zimesababisha vifo vya watu sita, nyumba 13 kusombwa na kaya 22 kuyahama makazi katika Kata ya Maore.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, wamefika eneo la tukio kuzungumza na wananchi huku mafundi wakiendelea na jitihada za kurejesha mawasiliano ya barabara katika daraja hilo.
Akizungumza na wananchi Babu amewaomba kuwa na subira wakati jitihada za kurejesha mawasiliano zikiendelea.
“Niwape pole kwa majanga haya. Serikali inafanya kila linalowezekana kuwanusuru wananchi wote mliokumbwa na maafa haya,” amesema Babu na kuongeza;
“Nimekuja kwa niaba ya Serikali kuwapeni pole, taarifa hizi, nimeshamjulisha Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) ambaye ofisini yake inajihusisha na masuala ya maafa, hivyo wale ambao nyumba zao zimebomoka na hawana makazi Serikali itakuja kuwasaidia.”
Aidha, amewaelekeza viongozi kuwahamasisha wananchi waliojenga katika maeneo yote hatarishi kuhamia kwenye maeneo salama ili kuepuka madhara zaidi, hasa kuelekea msimu wa mvua za masika.
“Nawaomba sana muwaelekeze watu wetu waliopo maeneo hatarishi, tafuteni maeneo yenye usalama wahamisheni hao, ili haya ya huku yabaki mashamba lakini wao waondoke huku waende kwenye maeneo tambarare, vinginevyo hizi ni mvua za vuli sasa bado za masika zikija itakuwa hatari nyingine kubwa,” amesema Babu.
Wakati huohuo, Babu ametoa mkono wa pole wa Sh3 milioni kwa familia sita zilizopoteza wapendwa wao katika maporomoko hayo.
Amesema kati ya fedha hizo, Sh700,000 zimetolewa kwa familia iliyopoteza baba na mama, Sh2 milioni kwa familia tano na Sh300,000 kwa manusura mmoja aliyelazwa hospitalini akiendelea kupatiwa matibabu.
“Kwa familia ambazo nyumba zao zimebomoka, Serikali itaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa hiyo niwape pole na niwahakikishie misaada zaidi itaendelea kutolewa,” amesema.
Naye Diwani wa Maore, Rashid Juma ameishukuru Serikali kwa hatua za haraka walizochukua kuwanusuru wananchi.
Amesema katika kata yake watu wawili wamefariki dunia, nyumba 13 zimebomoka na kaya 22 zimeyahama makazi yao kwa hofu ya mvua zinazoendelea wilayani humo.
Kuhusu daraja, diwani huyo amesema, “Daraja hili linaunganisha wananchi kutoka mikoa mbalimbali, hivyo kusombwa kwake kumewasababishia kuzunguka zaidi ya kilomita 60 ili kufika kwenye maeneo yao, jambo lililosababisha nauli kupanda.”
Akizungumzia mchakato wa urejeshwaji wa huduma za mawasiliano katika eneo hilo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani humo, Benitho Mdzovela amesema wamelazimika kujenga daraja la dharura ili kurejesha huduma hizo, akibainisha kuwa mawasiliano yatarejea ndani ya siku mbili.
” Tunaweka kalavati za muda ili kuchepusha maji na kuimarisha ukuta wa daraja wakati wa kipindi hiki cha mvua,” amesema Mdzovela.
Kwa upande wao, Lovenes Julius na Dickson Msuya, ambao ni wakazi wa Kijiji cha Mpirani, wamesema kutopitika kwa daraja hilo kunawasababishia usumbufu mkubwa na sasa wanalazimika kutumia njia ndefu kufika kwenye makazi yao.
Wameiomba Serikali kuhakikisha inajenga daraja imara ambalo halitasababisha maafa ya mara kwa mara, wakisisitiza kuwa daraja hilo limewahi kusombwa na mafuriko zaidi ya mara moja.