Moshi yafurika, wafanyabiashara walia hali ngumu

Moshi. Zikiwa zimesalia saa chache kabla ya kuadhimisha Sikukuu ya Krismasi, mji wa Moshi umefurika wageni kutoka maeneo mbalimbali waliokuja kusherehekea Krismasi na Mwaka Mpya pamoja na familia zao.

Hali hii imeongeza msongamano mkubwa wa watu na magari kwenye barabara kuu za mji huo.

Barabara zenye msongamano ni za katikati ya mji wa Moshi kama Nyerere, Sokoni, Boma, Kristu Mfalme, Rindilane, Stesheni, na barabara kuu ya Njiapanda ya Himo-Arusha.

Msongamano huu unatarajiwa kuendelea hadi jioni leo jioni wakati watu wengi wakitarajiwa kuelekea vijijini kwa ajili ya kusherehekea sikukuu hiyo.

Licha ya ongezeko la wageni, baadhi ya wafanyabiashara katika Soko la Mbuyuni wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Desemba 24, 2024, wamelalamikia hali ngumu ya biashara huku wakitaja mzunguko mdogo wa fedha ni moja ya changamoto kwao.

Mohamed Mfinanga, mfanyabiashara wa matunda amesema mauzo yamepungua kwa kiasi kikubwa huku matunda yakiharibika sokoni kutokana na ukosefu wa wanunuzi.
“Matunda hayatoki kabisa. Unaweza kununua ukashangaa yanaharibika baada ya siku tatu au nne. Wiki nzima imekuwa ngumu sana. Labda watu wamehamia kununua nguo za sikukuu na wakishamaliza jioni hii wanapanda vijijini,”amesema Mfinanga.

Naye Ibrahim Mohamed, mfanyabiashara wa nafaka amesema bado biashara ni ngumu licha ya kushusha bei za bidhaa.
“Mwaka huu hela ya mzunguko ni mdogo sana, ndiyo maana wanunuzi nao wamepungua. Tofauti na mwaka jana, sasa hivi mauzo ni kidogo sana,”amelalamika Ibrahim.

Mfanyabiashara mwingine wa nguo kutoka Dar es Salaam, Eva Mwase amesema hata baada ya kushusha bei za nguo za watoto, bado wanunuzi hakuna.
“Kipindi cha nyuma kuanzia Desemba 18 hali sokoni ilikuwa nzuri. Nimepunguza bei kutoka Sh20,000 hadi Sh10,000, lakini bado wateja hawapo,”amesema Mwase.

Changamoto kama hiyo pia imewakumba wafanyabiashara wa viatu, Gasper Mushi amesema faida yake ya kila siku imepungua sana.
“Miaka ya nyuma nilikuwa napata faida ya Sh30,000 hadi Sh35,000 kwa siku, lakini sasa hata kupata Sh10,000 ni shughuli,” amesema Mushi.

Hata hivyo, hali ni tofauti kwa Lilian Temba, wakala wa huduma za kifedha, ambaye amesema miamala imeongezeka tangu Desemba 20, 2024.
“Watu wengi sana wanafanya miamala, tofauti na kipindi cha nyuma. Hii imesaidia biashara yangu kuwa nzuri mwaka huu,” amesema Temba.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Mbuyuni, Lameck Mziray amesema licha ya changamoto ya upungufu wa nyanya na tangawizi, bidhaa nyingine zipo sokoni kwa bei nafuu.
“Tangawizi imepanda bei kutoka Sh2,000 hadi Sh5,000 kwa kilo, lakini bidhaa nyingine zipo fair. Tunadhani kupungua kwa biashara mwaka huu kunatokana na hali ya uchumi,” amesema Mziray.

Pamoja na changamoto hizi, mji wa Moshi unaendelea kushuhudia msongamano mkubwa wa watu na magari, huku sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya zikiendelea kuleta hamasa na shamrashamra mjini humo.

Related Posts