Ahoua aibeba Simba ikijiimarisha kileleni

SIMBA imeokota pointi tatu zingine ngumu kwenye mchezo uliotoa mshindi dakika za jioni ikiichapa JKT Tanzania kwa bao 1-0, ushindi ukiendelea kuwaweka kileleni katika sikukuu ya Krismasi inayoadhimishwa kesho Jumatano Desemba 25.

Bao la kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Awesu Awesu akilifunga dakika ya 90+5 kwa mkwaju wa penalti baada ya Mohammed Bakari kumvuta beki Shomari Kapombe wakati akiwania pasi ya mfungaji wa bao na mwamuzi kuamua iwe penalti.

Haikuwa penalti pekee kwani Bakari akatolewa nje na mwamuzi Kefa Kayombo kutoka Mbeya akionyeshwa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu kisha Ahoua kuwaondoa kwenye presha mashabiki wa timu yake ambao walidhani kama mechi hiyo itamalizika kwa suluhu.

Ushindi huo unaifanya Simba kuendelea kujitanua juu ya msimamo ikifikisha pointi 37 baada ya kucheza mechi 14 ikishinda mechi 12 kati ya hizo.

Bao hilo la Ahoua linakuwa la saba msimu huu akiendelea kuwa na muendelezo mzuri wa kufunga akiwa kinara wa mabao kwenye timu hiyo akifuatiwa na Leonel Ateba mwenye mabao matano.

YAKUBU MTATA
Simba ilifanya kila jitihada za kuutafuta ushindi lakini kama kilikuwa na mtu mtata aliyetishia ushindi wao kwenye mchezo huo alikuwa kipa wa JKT Tanzania, Yakubu Seleman ambaye alikuwa imara langoni kwake akiokoa mashambulizi makali ya wekundu hao.

Yakubu alipangua mashambulizi 11 ya Simba kupitia kwa Elie Mpanzu, Ateba na Ahoua ambayo kama sio uimara wake Wanajeshi hao wangepoteza vibaya.

MPANZU ANAJITAFUTA
Winga wa Simba, Mpanzu ameendelea kujitafuta akicheza mechi yake ya pili ambapo mpaka anatoka dakika ya 59 alionyesha kiwango kikubwa akifanya majaribio manne kwa mashuti ya mguu wa kushoto na kulia lakini Yakubu akamgomea katakata.

BOCCO VS SIMBA
Mshambuliaji wa JKT Tanzania, John Bocco jana alicheza kwa mara ya kwanza dhidi ya timu yake za zamani ya Simba akitumika kwa dakika 13 za kawaida na zile sita za nyongeza.

Bocco ambaye ni nahodha wa zamani wa Simba, hata hivyo hakuwa na madhara yoyote dhidi ya waajiri wake wa zamani kutokana na timu yake kucheza nyuma zaidi ikijilinda kwa muda mrefu wa mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex pale Mwenge jijini Dar es Salaam.

Related Posts