Babati. Askari polisi wa Kituo cha Kibaya wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, Geogre Mwakambonjo (40) amefariki dunia baada ya kugongwa na lori alipokuwa amepanda kwenye pikipiki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Ahmed Makarani amesema tukio hilo limetokea leo Jumanne Desemba 24 mwaka 2024.
Kamanda Makarani ameeleza kuwa askari polisi huyo amefariki dunia baada ya kugongwa na lori akiwa amepakizwa kwenye pikipiki.
Ameeleza kuwa, askari polisi huyo, amepata ajali hiyo eneo la Msasani, Kata ya Maisaka mjini Babati kwenye barabara kuu ya Arusha – Dodoma.
Kamanda Makarani amesema chanzo cha kifo cha askari huyo ni uzembe wa dereva aliyekuwa anaendesha lori kwa kutokuwa makini.
“Ajali hiyo imetokea baada lori lililokuwa nyuma ya pikipiki hiyo kumgonga mwendesha pikipiki kwa nyuma na kusababisha kifo cha askari polisi huyo,” amesema Kamanda Makarani.
Amesema polisi huyo aliyekuwa amebebwa na pikipiki alifariki dunia papo hapo.
Mmoja kati ya shuhuda wa tukio hilo, Alexander Ombay amesema uzembe wa dereva wa lori umesababisha kutokea kwa kifo hicho.
“Ajali hiyo imetokea baada ya lori lililokuwa nyuma ya pikipiki hiyo kumpigia honi hali iliyosababisha kupoteza uelekeo na kumgonga kwa nyuma,” amesema Ombay.
Wakati huohuo, Kamanda Makarani amesema hali ya ulinzi na usalama katika mkoa huo imeimarishwa na kuwataka watu kusherehekea Sikukuu ya Krisimasi kwa amani na utulivu.
“Hata hivyo, ulinzi unaanzia kwako mwenyewe watu wanapotoka nyumbani wahakikishe wanaacha mtu nyumbani kwa ajili ya usalama ili kusitokee wizi,” amesema.
Amesema wamejipanga kuhakikisha usalama unakuwepo kwa kuwapanga askari polisi na askari kanzu kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo ili kuimarisha ulinzi.