Dar es Salaam. Saa 48 za mkutano wa wadau wa demokrasia nchini ulikuwa moto ambapo hoja nzito ziliibuliwa, baadhi ya wadau kunyoosheana vidole, wengine kutaniana na mwisho wa mkutano huo kutoka na maazimio ya pamoja.
Mkutano huo uliofanyika Mei 8 na 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam ulilenga kutafakari na kujenga uelewa wa pamoja juu ya sheria za uchaguzi zilizopitishwa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu. Mkutano huo uliandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wastaafu, vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na wananchi wengine walijitokeza kusikiliza majadiliano hayo.
Hoja lukuki ziliibuliwa wakati wadau hao wakieleza uelewa wao kuhusu sheria za uchaguzi zilizopitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kisha kuanza kazi rasmi, huku baadhi ya wadau wakihoji kuchelewa kwa kanuni za sheria hizo ilhali uchaguzi wa serikali za mitaa umekaribia.
Sheria hizo ni Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Sheria ya Vyama vya Siasa. Wadau waliweza kuchimba na kueleza namna sheria hizo zitakavyochochea kuwa chaguzi huru na za haki.
CCM yanyooshewa kidole
Katika mkutano huo, viongozi mbalimbali wa CCM walihudhuria na kushiriki mjadala huo. Ujumbe wa CCM uliongozwa na Naibu katibu mkuu (Bara), John Mongella, pia alikuwepo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Mary Chatanda.
Vilevile, alikuwepo Hawa Ghasia, ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa UWT pamoja na Mbunge wa Kilosa (CCM), Profesa Palamagamba Kabudi, ambaye kwenye mkutano huo ndiye alizungumza kwa niaba ya chama hicho tawala.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alianza kwa kukirushia lawama chama hicho kwa kusema ndicho kimelifikisha Taifa hapa lilipo kwa sababu ya yote kilichoyafanya kwenye chaguzi za mwaka 2019 na 2020, na kusababisha kutungwa kwa sheria hizo.
Alisema imepita zaidi ya miaka 30 sasa, Watanzania wanajadili mambo yaleyale, lakini hakuna jambo la maana linalofanyika kwa sababu CCM ni wanufaika wa upungufu wote unaolalamikiwa na ndiyo maana hawataki kufanya mabadiliko.
Alisisitiza kwamba hata wangefanya mabadiliko makubwa ya sheria kiasi gani, kama upande wa pili wa CCM hawana utashi wa kisiasa, hayo mabadiliko itakuwa ni kupoteza muda kwa sababu hawako tayari kubadilisha mambo yanayowanufaisha.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Maftah Nachuma alisema Watanzania wamekuwa wakiambiwa na Rais Samia na viongozi wengine kwamba sasa ni wakati wa kujenga Tanzania mpya na kusahau yaliyotokea huko nyuma.
“Kwa wasiokumbuka, mwaka 2019 na 2020, asilimia 90 ya wagombea wa upinzani waliambiwa hawajui kusoma na kuandika, wakaenguliwa, wenzetu wa CCM walifanya haya kwa makusudi kabisa,” alisema Nachuma.
Hata hivyo, mwakilishi wa CCM kwenye majadiliano hayo, Profesa Kabudi alisisitiza kwamba kuna umuhimu wa kuwa na tafakari ya pamoja kuhusu mustakabali wa Taifa, huku akisisitiza kwamba hatua kubwa imepigwa kwenye masuala ya sheria na chaguzi nchini.
“Kwa CCM mabadiliko yote yaliyofanyika hayajafika ukomo na huu ni mchakato, ni mwendo, ni safari, unamwagilia maji ili mmea ukue, kwa hiyo yapo mengi ya kufanyiwa kazi, lakini hatua iliyochukuliwa ni sahihi na mwendo sahihi,” alisema Profesa Kabudi.
Kijana achafua hali ya hewa
Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Twaha Mwaipaya alisema alicha, 2fua hali ya hewa katika ukumbi wa mkutano huo aliposema vijana wapewe nafasi ya kuleta mabadiliko kwa njia mbadala, kwa kuwa bila hivyo hawatapata mabadiliko wanayoyataka.
“Haya yote yanafanyika kwa sababu vijana wa Tanzania hatujatambua nguvu yetu wenyewe. Ukiangalia mchakato wa uchaguzi kwenye mitaa yetu, anayesimamia uchaguzi ni mtendaji, anamtangaza diwani.
“Watanzania tukiijua nguvu yetu tutaacha kulalamika na kwa kuwa Serikali ya CCM haisikilizi, tutaongea hapa hadi asubuhi. Kama tumelalamika kwa miaka 30 kuhusu hizi sheria, hata tukiwapa miaka 50 hawawezi wakabadilisha
“Cha msingi, lazima tuone namna nyingine ya kwenda kukabiliana na huu mfumo, nje ya kuwaza hizi sheria, kwa sababu kwanza hawana polisi, magereza na mahakama za kutosha. Tukibuni njia mbadala za kukabiliana nao, hawa wanakwenda kuachia dola.”
Kauli hiyo ilimsimamisha Askofu wa Kanisa la Uamsho la Moravian, Emmaus Mwamakula ambaye alisema vijana wako wengi nchini, hivyo maoni yao kama hayo siyo ya kupuuzwa kwa sababu yanawakilisha kundi hilo na hasira walizonazo.
“Tusidharau kauli za vijana hawa, wanaosoma historia, wanakumbuka Adolf Hitler alivyoanza kama kijana, akaenda, akabadilisha mfumo. Ile ni kauli ya watu ambao wamekuwa frustrated (wamevurugwa) na sisi tuko hapa tusidharau,” alionya askofu huyo.
Hoja ya Ghasia ilivyozimwa
Suala jingine lililojitokeza ni ushauri uliotolewa na mbunge wa zamani wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia aliyewataka washiriki wa mkutano kujikita katika vifungu mahususi katika kutoa mchango wao kwa mada husika.
“Naomba nitoe ushauri kwa mwendesha mjadala (Jebla Kambole), tunajadili sheria, bahari nzuri tumepewa, kwa hiyo utuongoze twende kifungu kwa kifungu kama sheria inavyojadiliwa, lakini tukisema tujadiliane tu kama tuko kwenye mkutano wa hadhara tutaondoka ng’ombe bado hajanenepa.
“Tujadili mtu akisimama aende moja kwa moja aseme, tafsiri au kitu fulani hakijakaa sawa, napendekeza hivi hapo tutamaliza, lakini tukikaa na kuanza sijui mtu alinyang’anywa kadi wakati akienda kutoa ‘copy’ na mwingine alishikwa njiani, tutafika mwisho hatujapata chochote wala sheria ya mfano,” alisema Ghasia.
Ushauri huo wa Ghasia, aliyewahi pia kuwa Waziri wa Tamisemi katika serikali ya awamu nne, uliibua mjadala kwa washiriki wa mkutano waliotaka waachwe huru kuchangia sheria iliyowasilishwa bila kutakiwa kujikita kwenye vifungu mahususi.
Ni kama vile Kambole ambaye kitaaluma ni mwanasheria alivyoupokea ushauri huo wa Ghasia, akiwataka washiriki watakaopewa kipaza sauti kujikita kwenye vifungu maalumu.
Hata hivyo, kama vile somo hilo halikueleweka kwa baadhi ya washiriki wa mkutano huo, ambapo aliposimama mbunge za zamani wa Rombo mkoani Kilimanjaro, Joseph Selasini alisema yeye ana maoni ya jumla katika mada iliyowekwa mezani.
“Mtanisamehe, kama tulivyokubaliana jana kila mtu achangie kwa uhuru kile anachokifiria,” alisema Selasini.
Wakati Selasini akieleza hayo, mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, Suzan Kiwanga alisema mwaka 2020 alifanyiwa figisu za kutoteuliwa na mkurugenzi wa uchaguzi wa jimbo la Mlimba, licha ya kuwa na sifa zote zinazotakiwa.
“Mwaka 2020 kilinipata kilichonipata, kinyume na utaratibu wa Katiba na sheria za nchi, nilifanya taratibu zote na kulipa ada, hadi saa moja usiku hakuniteua, leo mnavyosema tujadili hii sheria kifungu kwa kifungu kama niko bungeni hii hapana, bora mninyang’anye kipaza sauti.
Kiwanga, aliyewahi kuwa mbunge wa Mlimba mkoani Morogoro, aliwataka washiriki hao kuwa makini katika kuchangia na kujadili ili kuweka kumbukumbu sawa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Vijembe vyatawala
Baada ya hapo vijembe vikaanza kwa Kiwanga kusema alishiriki baadhi ya vikao wakati mke mwenzake (Ghasia), akiwa Waziri wa Tamisemi, akisema vyama viliitwa kutengeneza kanuni, lakini zililetwa dakika za mwisho.
“Wakati wadau wanatoa maoni kama ya haya kuboresha kanuni wanayachukua, lakini kumbe wameshaziandaa, halafu dakika ya mwisho karibu na uchaguzi wanawaita,” alisema Kiwanga.
Ghasia alijibu mapigo akisema: “Sheria tunazozijadili ni za mfano zilizoandaliwa na TCD na sio Serikali au CCM. Suzani Kiwanga ni mke mwenzangu, yeye ndiye aliyekuja kwa mume wangu, mimi nilikuwa wa kwanza kuolewa halafu yeye akafuata, lakini ana wivu zaidi kushinda mimi niliyemkaribisha.
“Yale ya mwaka 2020, hata mimi yalinikuta, lakini mwenzako nimeshamaliza kulia na maisha yanaendelea na wewe maliza ili ujiandae na mwaka 2025,” alisema Ghasia.