Baba aliyefungwa kwa kuzini na mwanaye aachiwa huru

Sumbawanga. Ni mtihani mzito, ndivyo unavyoweza kueleza baada ya baba aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kuzini na mwanaye wa kumzaa, kuachiwa huru na Mahakama ya Rufani Tanzania.

Inaweza kusemwa ni mtihani kwa sababu mama mzazi wa mtoto alisimama bega kwa bega na mumewe na akatoa ushahidi akiwa ni shahidi wa pili wa utetezi mahakamani, huku akisisitiza mumewe hajawahi kufanya ufedhuli huo na kutaka aachiwe huru.

Awali, mume huyo alishtakiwa kwa makosa mawili, moja la kuzini na maharimu na lingine la kumpa ujauzito. Kwa kosa la kuzini na mwanaye alifungwa maisha na la ujauzito alifungwa miaka 30.

Hata hivyo, alikata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania na jaji aliyesikiliza rufaa hiyo, alibariki kosa la kuzini na mwanaye, lakini akapunguza kifungo cha maisha jela na kuwa cha miaka 30.

Jaji alisema kosa la kumpa ujauzito mwanaye lilikuwa halijathibitishwa, hivyo kubatilisha kutiwa kwake hatiani kwa kosa hilo, ndipo akakata rufaa kupinga kutiwa hatiani kwa kosa la kuzini na mwanaye na kushinda.

Katika hukumu iliyotolewa juzi, Desemba 23, 2024 na jopo la majaji watatu, Barke Sehel, Dk Paul Kihwelo na Gerson Mdemu, wamethibitisha upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha shtaka hilo la jinai.

Mwathirika wa tukio hilo ni mtoto wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Majengo katika wilaya ya Mpanda na tuhuma za kuzini na baba yake mzazi zinadaiwa kutendeka kati ya Januari mosi, 2017 hadi Aprili 29, 2019.

Ilidaiwa Aprili 29, 2019, kaimu mwalimu mkuu wa shule hiyo aliwapima ujauzito wanafunzi wa kike walirudi shule baada ya likizo na watoto tisa walipimwa.

Upimaji huo uliofanyika zahanati ya Sabato, mtoto huyo alibainika kuwa na ujauzito wa miezi mitano na ndipo ofisa ustawi wa jamii alipompeleka Polisi, huko ndipo alimtaja mhusika ni baba yake.

Baadaye alieleza wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo kuwa uhusiano wao wa kimapenzi na baba yake ulianza mwaka 2017 na siku moja baba yake alirudi akiwa amekunywa pombe na kumtaka avue nguo.

Ilielezwa baba yake akampaka dawa ya mitishamba usoni, akavua nguo na kuingiza uume wake na tangu siku hiyo waliendelea na uhusiano huo.

Njia ya mwasiliano baina yao ilikuwa ni kwa  meseji za kuandika kwenye karatasi na mmoja anapotaka kuwasiliana na mwenzake anaadika ujumbe katika boksi ambalo lilihifadhiwa karibu na mlango.

Hivyo baba au mtoto alikuwa akitembelea boksi hilo mara kwa mara na kusoma ujumbe wa mwenzake, kisha kuujibu na kwamba walikuwa wakifanya mapenzi wakati mke wa mwanaume huyo akiwa amesafiri.

Uchunguzi wa mwandiko wa wawili hao ulifanywa na kitengo maalumu cha utambuzi cha Polisi (IB) na ndipo mwanamume huyo akakamatwa, lakini mkewe akamtetea kuwa yeye (mke) hakuna siku aliwahi kusafiri.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa jamhuri na ule wa mshtakiwa, Mahakama ya Wilaya ya Mpanda ilimtia hatiani kwa makosa mawili ya kuzini na mwanaye na kumpa ujauzito na ndipo akaamua kukata rufaa.

Mahakama ya rufani iliegemea sababu kuu mbili, moja ni kuwa mahakama kuu iliyobariki kutiwa kwake hatiani kwa kosa la kuzini na mwanaye ilikosea kisheria kwa kuwa jamhuri haikuthibitisha kosa hilo.

Hoja ya pili ni kuwa mahakama hiyo ilikosea kisheria kuhusiana na hoja ya uchambuzi na kupima ushahidi wa pande zote mbili pale ilipotizama ushahidi wa jamhuri pekee na ulijaa matundu mengi na mashaka.

Katika hukumu yao, majaji wa Mahakama ya Rufani walisema ili kosa la kuzini na maharimu lithibitishwe, ni lazima kwanza kuwepo na uhusiano wa baba mtoto na pili kuwepo na kufanyika kwa mapenzi baina ya wawili hao.

“Katika vigezo hivyo viwili, upande wa mashtaka ulithibitisha kupitia ushahidi kuwa mrufani ni baba mzazi wa mwathirika. Hili liko wazi kwa ushahidi wa upande wa jamhuri na wa utetezi,” walisema majaji hao.

Hivyo, majaji wakaenda katika hoja ya pili ya malalamiko kuwa ushahidi haukufanyiwa uchambuzi makini, hasa ushahidi wa mtoto aliyekuwa shahidi wa pili (mtoto) ambao mahakama ndio iliyouamini zaidi.

Majaji hao walisema uaminifu huo pamoja na ushahidi mwingine upo katika mawasiliano ya meseji kati ya mrufani na mwathirika na walinukuu neno kwa neno katika moja ya mawasiliano yao hayo.

Ujumbe unasomeka, “Tusifanye leo kwa sababu haujacheza. Tutafanya kesho unahema sana atasikia mama yako” mtoto akajibu, “sawa tusifanye”.

Katika ujumbe mwingine anasomeka “Halafu tabia mbaya nilishakukataza, angalia nitakumaliza…Sitaangalia wewe ni mtoto wangu”, mtoto naye akajibu, “mimi nimekuelewa…sawa”, mwisho wa kunukuu jumbe hizo.

Majaji hao walisema mahakama zote za chini zilitumia jumbe hizo kuthibitisha kulikuwepo na tendo la ngono kati ya baba na mtoto, lakini kiuhalisia hazithibitishi wawili hao kufanya mapenzi.

“Tunafikiri hakimu pamoja na jaji walizidisha. Makosa ya kubaka, kulawiti na kuzini na maharimu yanahitaji uwepo wa mwingiliano (penetration). Uume wa mwanamme kuingia kwa uke wa mwanamke,”walisema.

Majaji hao walisema ujumbe uliokuwepo kwenye boksi ukisema “Tufanye kesho, unahema sana mama yako atasikia” au “tufanye leo mara moja na kesho”, hauthibitishi mrufani kumwingilia mtoto wake huyo.

“Hayo yanaweza kuashiria jambo lingine kabisa ambalo sisi hatutaki kuleta porojo.Tunachoweza kusema jumbe hizo zilizokuwa kwenye boksi  kwa viwango vyovyote vile havithibitishi mrufani kumwingilia mtoto,”walisema.

Majaji wakanukuu sehemu nyingine ya ushahidi ambapo mtoto alinukuliwa akisema walikuwa wakifanya mapenzi chumbani wakati ndugu wengine wakiwa wamelala na wakati mama yake hakuwepo.

Sehemu nyingine inasema “Ulinikamata na wavulana wawili, ninafahamu wanapoishi. Ninawafahamu marafiki zangu hao wa kiume, lakini sikuwahi kufanya nao mapenzi. Sina rafiki mwingine wa kiume zaidi ya baba”

Majaji walisema kwa kutizama kwa ukaribu ushahidi huo wa mtoto, mambo mengi yanaibuka na mtu anaweza kuhoji inakuwaje baba na mtoto wafanye mapenzi katika chumba ambacho wapo watoto wengine pia.

“Idadi ya watoto hao wengine na umri wao haukuelezwa, lakini baadaye alibadili na kusema alikuwa akifanya mapenzi na baba yake wakati mama yake amesafiri. Lakini mama anakana kuwahi kusafiri,” walisema.

Majaji walisema kwa ushahidi huo, mahakama iliyosikiliza shauri hilo ilitakiwa isimwamini mtoto huyo aliyekuwa shahdi wa pili wa jamhuri, hivyo wanakubaliana na mrufani kuwa jamhuri haikuthibitisha shtaka.

Kutokana na msimamo huo, majaji wakasema wanaona rufaa hiyo ina mashiko, hivyo wanabatilisha kutiwa kwake hatiani na adhabu aliyopewa na kuamuru aachiwe mara moja kutoka gerezani, isipokuwa kama anashikiliwa kwa makosa mengine.

Related Posts