Watanzania wahimizwa kusoma vitabu wapate mbinu kukua kiuchumi

Dar es Salaam. Watanzania wametakiwa kuwa na utamaduni wa kujisomea vitabu kwa ajili ya kujiongezea maarifa ikiwamo mbinu za kujiendeleza kiuchumi.

Utamaduni wa kusoma vitabu utaondoa dhana iliyozoeleka kwamba, ukitaka kumficha Mwafrika maarifa, yaweke kwenye vitabu.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila wakati wa uzinduzi wa kitabu kiitwacho ‘I Am Positioned’ kilichoandikwa na mwandishi Leah Karunde, ambaye pia ni mshauri wa masuala ya kodi.

Kafulila amesema Taifa linaweza kuendelea kwa kuwa na watu wenye maarifa, licha ya kuwepo kwa rasilimali za kutosha.

“Kitabu hiki kina mambo mengi mazuri ikiwamo kuhusu uhuru wa kifedha, uwekezaji na nidhamu ya matumizi. Hivyo, ni vema watu wakakisoma kwa sababu kina mambo mengi ya kujifunza katika kujiendeleza kiuchumi.

“Tunahitaji kuwa na jamii yenye mtazamo chanya kuhusu masuala ya kifedha ili kuwa na nidhamu katika matumizi yake kwa kuwekeza maeneo mbalimbali,” amesema Kafulila.

Ameongeza kuwa, kuna fursa mbalimbali za kiuchumi zinazowekwa na Serikali akiwataka wananchi kuzichangamkia na kuongeza kuwa kitabu hicho ni sehemu ya mwongozo katika kuisadia jamii kufikia malengo ya kibiashara, nidhamu ya fedha na uwekezaji.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wasomi mbalimbali wakiwamo washauri wabobevu katika masuala ya kifedha, mwandishi Leah amesema kitabu hiki kinawajengea uwezo wa kifedha watu mbalimbali wakiwamo vijana katika kukuza uchumi katika ngazi binafsi, familia na jamii kwa ujumla.

“Kitabu hiki hakifundishi kuhusu pesa tu, bali pia kinafundisha namna ya kujiwekea malengo, ustahimilivu, maarifa yanayoweza kutumika katika kujenga misingi imara ya kifedha, kuunda vyanzo vingi vya mapato na kujifunza mbinu za kuokoa pesa na kuwekeza.

“Lakini pia, kina hadithi binafsi zinazoelezea namna ya kushinda changamoto mbalimbali na zinazoelezea changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana barani Afrika na kutoa ramani ya mabadiliko ya biashara za familia kuwa mashirika yanayostawi,” amesema Leah.

Amesema lengo ni kuwasaidia watu wengine, kupitia kitabu hicho na kuhamasisha jamii kufikia mafanikio ya kifedha katika kuunga mkono juhudi za Serikali kuboresha maisha kwa Watanzania.

Kwa takwimu za usomaji vitabu duniani,utafiti wa usomaji wa vitabu unasema asilimia 27 walisoma zaidi ya vitabu 20 mwaka 2022, asilimia 32 walisema walisoma kitabu kimoja hadi vitano huku asilimia 18 tu ndo walisema walisoma vitabu sita hadi 10 na asilimia 19 walisoma vitabu 11 hadi 20 mwaka huo.

Related Posts