Mikate yadimika Moshi, sababu yatajwa

Moshi. Kufuatia wingi wa watu waliokuja kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya mkoani Kilimanjaro, bidhaa aina ya mkate imeadimika katika maduka makubwa (supermarkets) mjini Moshi  na kusababisha adha  kwa watumiaji wa bidhaa hiyo.

Bidhaa hiyo ambayo hutumiwa na familia nyingi imekuwa adimu kuanzia jioni ya leo, Desemba 24, 2024 na baadhi ya watu waliofika katika maduka hayo hawakupata mikate.

Hata hivyo, Mwananchi Digital imepita katikati ya mji na kushuhudia maduka hayo yakiwa hayana mikate hali itakayowalazimu walaji hao kutumia njia mbadala.

Wakizungumza leo, Desemba 24, 2014 baadhi ya walaji wa bidhaa hiyo, wamesema wamezunguka maduka mbalimbali ndani ya mji wa Moshi lakini hawakupata bidhaa hiyo.

Rachel Msuya, mmoja wa wananchi wa Manispaa ya Moshi, amesema amejaribu kuzunguka maduka mbalimbali lakini hakufanikiwa kupata bidhaa hiyo.

“Nimezunguka maduka mbalimbali ya hapa mjini mkate hakuna, ukienda kwenye supermarket hii unaambiwa hakuna, ukiende kwingine ni hivyo hivyo, kesho itabidi niwapikie wanangu chapati japo wanapenda mkate zaidi,” amesema.

Mkazi mwingine wa Moshi, Jasmin Abdul amesema kutokana na bidhaa hiyo kuadimika atalazimika kutumia njia nyingine mbadala ili familia yake iweze kupata chochote kitu asubuhi.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mji huo, Joseph Amani amesema kuadimika kwa bidhaa hiyo kunatokana na ongezeko la watumiaji.

“Kwetu sisi ni neema, watu wameongezeka matumizi ya mkate yamekuwa ni makubwa, tumejitahidi kuongeza kadri ya uwezo wetu lakini kila ukileta mikate inaisha mapema,”amesema mfanyabiashara huyo.

Pamoja na mambo mengine, mji huo umeonekana kuwa na msongamano mkubwa wa magari na watu na katika barabara za ndani  zimeonekana kuelemewa na wingi wa magari na kusababisha foleni.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limesambaza askari wake katika maeneo mbalimbali ya mji huo ili kukabiliana na ongezeko la magari.

Related Posts