Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sostenes amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu 2025 kwa kugombea nafasi mbalimbali, huku akiwaonya kutokubali kununulika haki zao na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu.
Amesema nchi inahitaji viongozi wazalendo ili waongoze kwa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele na si kwa kuzingatia ya matakwa yao yasiyo kuwa na hofu ya kujali umma na kwa Mungu.
Akisoma waraka wa askofu huyo kwa waumini katika ibada ya mkesha wa Sikukuu ya Krismas, Padri Jacob Kahemele wa Kanisa la St Alban Posta Dar es Saalaam, amesema kwa kutambua umuhimu wa kupata viongozi bora ni lazima wahamasishane washiriki kikamilifu.
“Mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa Taifa letu, kwa ajili ya urais, wabunge na madiwani ni muhimu kuliombea taifa livuke salama lakini uchaguzi ufanyike kwa amani na haki.
“Ni muhimu waumini kuhamasishana kujitokeza kwa wingi kushiriki na miongoni mwetu mjitokeze kugombea nafasi mbalimbali na kupiga kura na tusipuuze na wala tusikubali kununuliwa haki zetu na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu.” amesema Askofu.
Askofu katika waraka huo aliodai ataubandika kwenye mbao za matangazo ya Kanisa hilo, amesema taifa linahitaji viongozi wazalendo ili waongoze kwa kutanguliza maslahi ya taifa mbele na si kwa kuzingatia ya matakwa yasiyo kuwa na hofu kwa Mungu.
“Lazima tutambue maslahi ya Taifa ni muhimu zaidi kuliko itikadi au maslahi ya mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu wachache, siasa njema ni muhimu,” amesema
Amewataka Watanzania kuepuka siasa za chuki, ubinafsi na zinazolenga kuwagawanya kwa kuzingatia itikadi za udini na hata ukabila.
“Malumbano yenye kujenga chuki na yenye kuchochea fujo hayatufai katika kulinda amani ya nchi yetu, Tanzania ina thamani kubwa ni muhimu kudumisha kwa kuwa na siasa safi na salama,” amesema
Katika waraka huo, amesema Watanzania ni muhimu kufahamu uchaguzi ni jambo la msimu litapita lakini maisha ni jambo linalodumu wakati wote vizazi kwa vizazi.
Askofu huyo katika waraka huo amerejea mwaka huu ulifanyika uchaguzi wa serikali za mitaa licha ya kuisha salama lakini amedai ulikuwa na kasoro zinazotakiwa kufanyiwa kazi ili uchaguzi mkuu ufanyike kwa haki.
“Mwaka 2024 tulikuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa tunashukuru uliisha salama yamkini kulikuwa na changamoto zilizojitokeza ni muhimu kwa mamlaka zifanyie kazi kwa kuboresha ili uchaguzi mkuu unaokuja ufanyike katika mazingira mazuri,” amesema