Tume ya Kupambana na Ufisadi ya Bangladesh ilisema Jumatatu kuwa imeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya ufisadi, ubadhirifu, na utakatishaji fedha katika mradi wa Kinu cha Nyuklia cha Rooppur, unaoungwa mkono na Rosatom, shirika la serikali ya Urusi.
Mkataba wa ujenzi wa vinu viwili vya umeme, kila kimoja kikiwa na uwezo wa megawati 1,200, ulisainiwa mwaka 2015.
Tume hiyo imedai kuwepo kwa ukiukwaji wa kifedha wa thamani ya takriban dola bilioni 5, unaomhusisha Hasina, mwanawe Sajeeb Wazed, na binamu yake ambaye ni waziri wa hazina wa Uingereza, Tulip Siddiq, kupitia akaunti za nje ya nchi.
Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alisema Siddiq amekana madai hayo na anaendelea kuaminiwa. Siddiq ataendelea na nafasi yake, msemaji huyo aliongeza.
Soma pia: Mahakama Bangladesh yatoa waranti wa kumkamata Sheikh Hasina
Mnamo Agosti, vyombo vya habari vya Bangladesh viliinukuu kampuni ya Rosatom ikikana madai ya awali ya ufisadi, ikisema imejikita kwenye uwazi, sera madhubuti za kupambana na ufisadi, na uwazi katika michakato yote ya manunuzi.
“Uwindwaji wa kisiasa”
Wazed, akizungumza kwa niaba ya familia, alisema wanakabiliwa na “vita vya kisiasa” nchini Bangladesh.
“Haya ni madai yasiyo na msingi kabisa na kampeni ya kutuchafliua jina. Familia yangu wala mimi hatujawahi kuhusika au kuchukua pesa kutoka kwa miradi yoyote ya serikali,” aliiambia Reuters akiwa Washington, anakoishi.
“Haiwezekani kufuja mabilioni kutoka kwenye mradi wa dola bilioni 10. Sisi pia hatuna akaunti za nje ya nchi. Nimeishi Marekani kwa miaka 30, na shangazi yangu pamoja na binamu zangu wameishi Uingereza kwa muda mrefu sawa. Tuna akaunti hapa, lakini hakuna yeyote kati yetu aliyewahi kuona kiasi hicho cha pesa.”
Reuters haikuweza kuwasiliana na Hasina, ambaye hajaonekana hadharani tangu kutoroka kwenda New Delhi mapema Agosti baada ya uasi wenye umwagaji damu dhidi yake nchini Bangladesh. Tangu wakati huo, serikali ya mpito imekuwa ikiendesha nchi.
Serikali ya Dhaka ilisema Jumatatu kuwa imeiomba India kumrudisha Hasina. New Delhi imethibitisha ombi hilo lakini ikakataa kutoa maelezo zaidi.
Wazed alisema familia haijafanya uamuzi juu ya kurudi kwa Hasina Bangladesh, na kwamba New Delhi haijamshauri kutafuta hifadhi mahali pengine.