Mahakama kuu ya nchi hiyo inayozungumza Kireno ilithibitisha Jumatatu kuwa chama cha Frelimo, ambacho kimekuwa madarakani tangu 1975, kilishinda uchaguzi wa urais wa Oktoba 9 ambao tayari ulikuwa umechochea wiki kadhaa za machafuko.
Jumla ya “matukio 236 ya vurugu kali yaliripotiwa” kote nchini, yakisababisha watu wasiopungua 25 kujeruhiwa, wakiwemo maafisa wa polisi 13, Waziri wa Mambo ya Ndani Pascoal Ronda alisema katika mkutano wa waandishi wa habari Jumanne usiku.
“Vikundi vya watu wenye silaha, wakitumia visu na silaha za moto, vimefanya mashambulizi dhidi ya vituo vya polisi, magereza, na miundombinu mingine,” alisema Ronda. Zaidi ya watu 70 wamekamatwa, aliongeza.
Mji mkuu wa Maputo, ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa hauna watu, ulikumbwa na mapambano kati ya waandamanaji na polisi, waandishi wa AFP walisema.
Polisi waliokuwa kwenye magari ya kivita walipiga doria katikati mwa mji huo, ambako mamia ya waandamanaji katika makundi madogo yaliyotawanyika walirusha vitu na kuwasha moto.
Vizuizi vya barabara vilivyotengenezwa kwa haraka vilichomwa moto Jumatatu jioni, na kufunika mji na moshi mzito muda mfupi baada ya mahakama kuthibitisha ushindi wa mgombea urais wa Frelimo, Daniel Chapo.
Soma pia: Msumbiji yasubiri uamuzi wa baraza la katiba kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais
Mpinzani mkuu wa Chapo, kiongozi wa upinzani aliye uhamishoni Venancio Mondlane, amedai kuwa uchaguzi ulighushiwa, na kuzua hofu ya ghasia kati ya wafuasi wa vyama pinzani.
Maduka, benki, supermarketi, vituo vya mafuta na majengo ya umma vilivamiwa, madirisha yake kuvunjwa na bidhaa kuporwa. Baadhi yalichomwa moto na kubakia vifusi vilivyokuwa vikitoa moshi.
“Hospitali Kuu ya Maputo inafanya kazi katika hali ngumu; zaidi ya wafanyakazi 200 hawakuweza kufika kazini,” mkurugenzi wake Mouzinho Saide aliiambia AFP, akiongeza kuwa karibu watu 90 walilazwa na majeraha.
Arobaini walijeruhiwa kwa risasi na wanne kwa visu, aliongeza.
Barabara kuu zinazoelekea Maputo na mji jirani wa Matola zilifungwa na vizuizi na matairi yanayowaka, huku barabara inayoelekea uwanja wa ndege wa Maputo ikiwa haipitiki kwa kiasi kikubwa.
Wakazi wengi wa eneo hilo walibaki nyumbani, huku wachache waliojitokeza wakifanya hivyo kuangalia uharibifu au kufanya ununuzi wa Krismasi na mwisho.
Siku ya Krismasi huwa na shughuli nyingi, lakini maduka na hata madogo ya mitaa yalikuwa yamefungwa, na kufanya mafuta na mkate kutopatikana.
Usafiri wa umma pia ulisimama, huku magari ya wagonjwa na yale ya mazishi pekee yakiwa barabarani.
Machafuko yaanza kaskazini mwa Msumbiji
Machafuko hayo yamesambaa hadi miji kadhaa kaskazini mwa Msumbiji, vyombo vya habari vya ndani viliripoti, na vurugu na uharibifu katika majimbo ya Cabo Delgado, Nampula, Zambezia, na Tete, ambako upinzani una ufuasi mkubwa.
Zaidi ya watu 100 tayari wamekufa katika vurugu za baada ya uchaguzi ambazo hazijawahi kutokea, huku hofu ya idadi hiyo kuongezeka ikiwa juu baada ya Mondlane kudai ushindi.
Wamsumbiji wanadai “ukweli wa uchaguzi,” alisema Mondlane katika ujumbe wa Facebook. “Lazima tuendelee na mapambano, tubaki wamoja na imara.”
Soma pia: Mondlane atishia kuanzisha vurugu kubwa Msumbiji
Uthibitisho wa matokeo ya uchaguzi Jumatatu ulifanyika licha ya madai ya ukiukwaji kutoka kwa waangalizi wengi.
Chapo alishinda kwa asilimia 65.17 ya kura, zaidi ya alama tano chini ya matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.
Katika Bunge la Kitaifa, Frelimo lina viti 171 kati ya 250, chini kwa viti 24 ikilinganishwa na tangazo la Oktoba.
“Venancio,” kama Mondlane anavyoitwa mitaani, alirudia madai yake katika ujumbe wa mitandao ya kijamii Jumanne kwamba mahakama ya kikatiba ilikuwa ikihalalisha “udanganyifu” na “fedheha kwa watu.”
“Tunataka kuunda Mahakama ya Katiba ya Watu, ambayo itamthibitisha Venancio Mondlane kama rais,” alisema kuhusu yeye mwenyewe.
“Nitaapishwa na kupewa madaraka,” aliongeza.
Chapo, ambaye anatarajiwa kuanza rasmi kazi katikati ya Januari, alionyesha msimamo wa upatanishi katika hotuba yake ya ushindi Jumatatu, akihaidi “kuzungumza na kila mtu,” wakiwemo wapinzani wake wakuu.