Wapinzani wa Simba Caf waanza kutimuana

UNAWEZA kusema kimeumana huko Tunisia kwa wapinzani wa Simba katika Kombe la Shirikisho Afrika, CS Sfaxien ambapo mashabiki wake waliendeleza fujo wikiendi iliyopita ambazo zimeshinikiza uongozi kupangua safu ya benchi la ufundi.

Kwa mujibu wa taarifa za redio maarufu nchini humo iitwayo Mosaique FM, uongozi ulianza mazungumzo wahusika juzi ili kumalizana kwa makubaliano.

Uamuzi huo umetokana na kufanya vibaya kwa timu hiyo hasa mechi tatu za mwisho ambapo imepoteza zote. Ikumbukwe kuwa CS Sfaxien walikiona cha moto Desemba 15 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo walijikuta wakichapwa mabao 2-1 na Simba.

Inaelezwa fukuto la kufutwa kazi kwa kocha mkuu Alexandre Santos lilikuwepo tangu walipopoteza mchezo huo na kilikuwa kipigo cha tatu katika hatua ya makundi, ikiwa ni siku saba tu tangu mashabiki wa timu hiyo wafanye fujo Kwa Mkapa, Desemba 22.

Jumapili walifungwa 2-1 katika Ligi Kuu ya Algeria wakiwa ugenini na Metlaoui, ndipo mashabiki walipoamua kufanya fujo kushinikizwa afutwe kazi.

Mashabiki hao waliishambulia timu, jambo lililowafanya viongozi kufanya uamuzi wa kuachana na Mreno huyo ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji na kuanza  mara moja mchakato wa kutafuta kocha mpya.

CS Sfaxien walikuwa wameanza pia mazungumzo ya kuvunja mkataba na wachezaji kadhaa waliosajiliwa katika dirisha la usajili la majira ya joto, ambao wameshindwa kuthibitisha viwango vyao, akiwemo kiungo wa Ureno, Pedro, na mshambuliaji wa Albania, Ruben Hebaj.

Kabla ya CS Sfaxien kukutana na Simba katika mchezo wa raundi ya nne ya Kombe la Shirikisho Afrika wa hatua ya makundi Januari 5, 2025, watakuwa na michezo mitatu mbele katika ligi ya ndani ambayo ni dhidi ya Stade Tunisien, Esperance Tunis na CA Bizertin.

Related Posts