KESHO Jumapili Singida Fountain Gate na Mashujaa FC zitakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu za matumaini ya kubaki Ligi Kuu Bara na kumaliza nafasi za juu kwenye msimamo zitakapokutana katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni.
Singida FG inakamata nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 25, ikiwa imepoteza mechi 10, sare saba na kushinda sita, huku Mashujaa ikiwa kwenye nafasi ya 14 na alama 22 ikipoteza mechi 11, sare saba na kushinda tano.
Timu hizo zilivuna alama moja katika mechi zilizopita, Singida FG ikiibana Ihefu 1-1 na Mashujaa ikisuluhu na Azam FC. Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Lake Tanganyika, Novemba 6, 2023, Singida ilipata ushindi wa mabao 3-1.
Timu zote mbili zimekuwa na udhaifu kwenye safu za ulinzi na nyavu zao kutikishwa mara nyingi, ambapo Singida imefungwa mabao 31 na kufunga 20, huku Mashujaa ikifunga 19 na kuruhusu 19, hivyo kila moja ina nafasi ya kupata ushindi kama itatumia udhaifu wa mwenzake.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake, Kocha wa Singida FG, Ngawina Ngawina amesema ni moja ya mechi ngumu kutokana na matokeo yasiyo mazuri kwa timu zote mbili, huku akitamba kuwa alama moja waliyoipata dhidi ya Ihefu imewapa morali wachezaji wake.
“Morali ya vijana iko juu wapo tayari na wana kiu ya kupata pointi tatu, tumefanya maandalizi mazuri na wapo tayari kupata ushindi. Tumewaona Mashujaa na wao wametuona mwenye mbinu nzuri atapata matokeo,” amesema Ngawina
Ameongeza: “Nawapongeza vijana wanatengeneza nafasi tunaendelea kulifanyia kazi suala la kufunga. Suala la kufunga ni mtu binafsi mwalimu hakufundishi kufunga, mwalimu anafundisha kutengeneza nafasi.”
Kipa wa timu hiyo, Benedict Haule, amesema: “Wachezaji tunajua nafasi tuliyopo siyo tuliyoizoea, kwa hiyo tunapambana kwa uwezo wetu tukae katika nafasi za juu na tunaamini katika mechi zilizobaki tutapambana kuhakikisha tunaipeleka timu pazuri.”
Naye Kocha Msaidizi wa Mashujaa, Makatta Maulidi amesema katika nafasi waliyopo kila mchezo kwao ni kama fainali.
“Tunahitaji alama tatu na siyo kitu kingine, wachezaji wote wako salama na tuko tayari kwa mchezo wa kesho na kupata matokeo mazuri,” amesema Makatta.
Mchezaji wa timu hiyo, Shadrack Ntabindi amesema, “tumejiandaa vizuri mwalimu ameshafanya kazi yake kilichobaki ni sisi kutekeleza na kupata ushindi. Tunapambana kujinasua katika msimamo tunahitaji ushindi kesho kuhakikisha tunasogea kwenye nafasi za juu.”