YANGA ina rekodi nzuri inapocheza dhidi ya Dodoma Jiji katika mechi za Ligi Kuu Bara kwani haijawahi kupoteza tangu zianze kukutana Desemba 19, 2020.
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic analitambua hilo, lakini ametoa kauli ambayo inaashiria hataki kutembelea rekodi hiyo, zaidi kuona mapambano zaidi.
Ramovic ambaye huo utakuwa ni mchezo wa nne katika ligi tangu atambulishwe Novemba 15, 2024, amesema lazima wachezaji wajitoe kupambana ili ushindi upatikane huku akibainisha kuwa ratiba kwa sasa imekaa kimtego.
“Ushindi wa kesho (leo) unabeba dhima nzima ya kujitoa kwa kila namna. Kama tusipojitoa kwa kila hali kesho (leo), matarajio ya ushindi yatakuwa madogo. Kimsingi tumekuja hapa (Dodoma) na tumeshajiandaa sawasawa na tuna imani ya kuondoka na alama tatu.
“Bila shaka mchezo umekaa kimtego kutokana na ratiba lakini hiyo haiondoi dhamira yetu ya kushinda,” alisema Ramovic ambaye tayari ameonja ushindi katika mechi tatu za ligi zilizopita akishinda 2-0 ugenini dhidi ya Namungo na nyumbani akizichapa Mashujaa (3-2) na Tanzania Prisons (4-0).
Katika takribani siku 10, ratiba inaonyesha Yanga inatakiwa kucheza mechi nne ambapo Desemba 19 ilipambana na Mashujaa kisha Desemba 22 dhidi ya Tanzania Prisons, leo na Dodoma Jiji ilhali Jumapili Desemba 29 ni dhidi ya Fountain Gate.
Ratiba hiyo inamuumiza kichwa Ramovic huku akipambana kuuepuka mtego wa kudondosha pointi.
Yanga inaingia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma saa 10:00 jioni kukabiliana na wenyeji wao Dodoma Jiji.
Mikakati ya Ramovic ni kuhakikisha mzunguko wa kwanza wakimaliza, basi hata ikitokea wamezidiwa pointi siyo kwa pengo kubwa libaki tofauti ya pointi moja.
Katika kufanikisha hilo, Ramovic ameonekana kufurahishwa na namna kikosi kinavyocheza hivi sasa baada ya kutoka kushinda mabao 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons huku wachezaji kadhaa akiwemo Djigui Diarra, Clatous Chama na Maxi Nzengeli wakikosekana.
Dodoma Jiji ambayo huo utakuwa mchezo wa 15 inafahamu kwamba Yanga ni wababe wao, lakini imejipanga kuondoa matokeo hayo.
Timu hiyo inayoshika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, inanolewa na Mecky Maxime ambaye msimu huu amefanikiwa kushinda mechi nne, sare nne na kupoteza sita huku mechi tano za mwisho nyumbani ikishinda tatu na kupoteza mbili. Kikosi kinaonekana kuruhusu mabao mengi (16) huku kikifunga 13.
“Mchezo hautakuwa mwepesi kutokana na mpinzani tunayekwenda kukabiliana naye lakini tumejipanga kuhakikisha hatupotezi,” alisema Maxime.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana nyumbani kwa Dodoma Jiji, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 yaliyofungwa na Maxi Nzengeli, Clement Mzize na Aziz Ki aliyefunga mawili.
Katika mchezo wa leo, Nzengeli hayupo kutokana na kuuguza majeraha, lakini Aziz Ki na Mzize watakuwepo kwani wamesafiri na kikosi.
“Tumewatazama kwa makini sana Dodoma Jiji, wanacheza vizuri wakiwa nyumbani, tunafahamu ni wagumu mno wanapocheza nyumbani hivyo tumeshajiandaa kukabiliana nao. Alama tatu kesho (leo) muhimu mno kwetu ili tuendelee kubaki kwenye mipango yetu,” alisema.
“Jambo zuri ni kwamba wachezaji tuliokuwa nao hapa ni wazima, hakuna ripoti ya majeruhi mpya ukiachana na wale waliokosekana mchezo uliopita kitu ambacho kinatupa matumaini ya kuendelea kufanya vizuri.”
Rekodi katika mechi nne za mwisho nyumbani kwa Dodoma Jiji dhidi ya Yanga, zinaonyesha timu hiyo imepoteza tatu mfululizo huku ikiambulia suluhu moja. Dodoma Jiji 0-4 Yanga, Dodoma Jiji 0-2 Yanga, Dodoma Jiji 0-2 Yanga na Dodoma Jiji 0-0 Yanga.
Mbali na hivyo, matokeo ya jumla kwenye ligi katika mechi nane walizokutana, Yanga imeshinda saba na sare moja huku mechi sita za mwisho zote ikishinda.
Matokeo yapo hivi; Dodoma Jiji 0-4 Yanga, Yanga 1-0 Dodoma Jiji, Yanga 4-2 Dodoma Jiji, Dodoma Jiji 0-2 Yanga, Dodoma Jiji 0-2 Yanga, Yanga 4-0 Dodoma Jiji, Dodoma Jiji 0-0 Yanga na Yanga 3-1 Dodoma Jiji.
Yanga msimu huu imeshinda mechi zote sita za ugenini ikifunga mabao nane ikilinda nyavu zake zisiguswe, hivyo mchezo wa leo itataka kuendelea kufanya vizuri wakati Dodoma Jiji nyumbani imeshinda nne na kupoteza mbili katika mechi sita ikifunga mabao saba na kuruhusu matano. Takwimu hizo zinaonyesha kwamba Yanga ni hatari inapokuwa ugenini lakini Dodoma Jiji nayo haina matokeo mazuri. Tusubiri tuone leo.
Kabla ya mchezo wa Dodoma Jiji dhidi ya Yanga, Fountain Gate watakuwa wenyeji wa Namungo kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kuanzia saa 8:00 mchana. Ni mchezo ambao wenyeji wanaingia wakiwa na rekodi bora dhidi ya wageni wao.
Fountain Gate ambayo hapo awali ilitambulika kama Singida Big Stars kisha kuitwa Singida Fountain Gate, ina rekodi ya kuifunga Namungo mara nne katika mechi tano walizokutana ikiwemo ya msimu huu ambapo Fountain wakiwa ugenini walishinda 2-0 huku sare ikiwa moja. Mchezo wa leo ambao ni mzunguko wa pili, unawapa nafasi Namungo kujibu mapigo lakini pia wenyeji wao watataka kuendeleza rekodi yao bora.
Katika msimamo wa ligi, Fountain Gate iliyocheza mechi 14, imekusanya pointi 20 ikishika nafasi ya sita kabla ya mechi za jana wakati Namungo ni ya 12 na pointi zake 14 ikishuka dimbani mara 15.