Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa amegusia matukio ya utekaji yanayoripotiwa nchini akisema, Watanzania wamepitia kipindi kigumu.
Amesema tangu azaliwe kwake hajawahi kusikia watu wakitekwa.
Amesema hayo leo Desemba 25, 2024 katika Kanisa la Azania Front, jijini Dar es Salaam wakati wa ibada ya Krismasi ya kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
“Ndugu zangu Watanzania tumepita katika kipindi kigumu, Mungu amekiondoa kipindi hicho. Tangu kuzaliwa kwangu sijawahi kusikia watu wakitekwa, lugha ya kutekwa inaleta hofu. Hata mtu akikusogelea kukusalimia.
“Juzi alikuja askofu mmoja akanishika kwenye gari saa moja hivi nikashtuka akaniambia shiii… nikamwambia vipi askofu,” amesema.
Askofu Malasusa amesema jambo kubwa sasa ni Watanzania kumuomba Mungu ili hali hiyo ikome.
“Wale wenye roho za kuwachukua watu na kuwahangaisha Mungu ashughulike nao, tuna hofu nyingi katika maisha. Hofu ya uchumi, hofu ya ndoa, ndoa nyingi zimeharibiwa na ma-best man (wapambe wa harusi) na watu wa karibu ni muhimu kijana kumshirikisha Mungu katika ndoa yako na kupenda wazazi,” amesema.
Pia, amesema uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024 uligubikwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Amesema endapo hatua hazitachuliliwa dhidi ya vitendo alivyoviona kutavuruga uchaguzi mkuu 2025.
Askofu Malasusa amesema kulikuwa na viashiria vingi vya uvunjifu wa amani ambavyo visipoangaliwa vitahatarisha amani katika uchaguzi ujao.
“Kupitia uchaguzi wa Serikali za mitaa kulikuwa na viashiria vingi ambavyo nimeviona kabisa vinaweza kuharibu amani kwenye uchaguzi ujao ni lazima waombaji tuombe,” amesema.
Amesema kuzaliwa kwa Yesu Kristo ambaye ni bwana wa amani ni muhimu wapigakura, wasimamizi wa uchaguzi na watia nia kuingia kwenye maombi kwani ili nchi iwe na amani ni lazima kumgeukia bwana wa amani.
Muumini wa kanisa hilo, Josephat Abraham amesema ni faraja kwa viongozi wa dini kukemea matukio yanayokwenda kinyume cha mafundisho ya Mungu.
“Kuzaliwa kwa Kristo maana yake tumefanyika wapya, naamini yale mabaya yaliyotawala miezi ya nyuma tunakwenda kuanza mwaka mpya ambao Mungu kwa uweza wake atakwenda kumaliza mabaya yote yanayotokea dhidi yetu,” amesema.
Agnes Christopher, amesema sikukuu ya Krismasi inapaswa kutumika kutenda mema na kuepuka maovu.