Ceassia wanaitaka nne bora WPL

UONGOZI wa Klabu ya Ceassia Queens kutoka Iringa, umempa kibarua cha kuhakikisha anamaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, kocha mpya wa timu hiyo, Ezekiel Chobanka aliyetua wiki chache zilizopita akitokea Alliance Girls ya Mwanza.

Ili kuhakikisha timu hiyo inamaliza katika nafasi nne za juu, inapaswa kuchuana vikali na wababe Simba Queens, JKT Queens na Yanga Princess walio katika vita ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kuiongoza Ceassia Queens katika mechi mbili, Chobanka alisema kutokana na maandalizi dhaifu mwanzoni mwa msimu uongozi unahitaji kumaliza kwenye nne bora kisha ujipange mwakani kuwania ubingwa.

“Nashukuru uongozi umenipokea vizuri na umejaribu kuniambia kwamba tujaribu kusukuma tuone kama tunaweza kupata zile nafasi nne za juu lakini hata kama ikishindikana kwa sababu maandalizi yao ya msimu hayakuwa mazuri ili tujiandae vizuri msimu ujao tuingie kwenye ushindani,”  alisema Chobanka.

Alisema baada ya kufika alibaini kikosi hicho kina upungufu eneo la ushambuliaji na kiungo, na tayari kwenye dirisha dogo uongozi umesajili straika kutoka TP Mazembe na kiungo wa Kampala City Council ambao wameshaungana nao.

“Uongozi uko makini ndiyo maana baada ya kufika nimewaambia baadhi ya mapendekezo na haraka wameyafanyia kazi, tayari wametuletea hao wachezaji ninao mazoezini na naona mchango wao ni mkubwa, kama tukiendelea hivi tunaweza kufanya vizuri,”  alisema.

Kocha huyo atakuwa na kibarua kigumu katika mchezo ujao dhidi ya waajiri wake wa zamani, Alliance Girls aliyoachana nayo wiki chache zilizopita.

“Tunacheza na timu yangu ya zamani, naelewa ugumu wao ulivyo vijana wanajitolea sana, najua itakuwa mechi ngumu lakini dakika 90 zitaamua,” alisema.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Wanawake Tanzania Bara, Ceasiaa Queens iliyocheza mechi tano, inashika nafasi ya tisa ikiwa ni ya pili kutoka chini baada ya kukusanya pointi sita sawa na Bunda Queens, Gets Program na Fountain Gate Princess zilizo juu yake.

Related Posts