Kocha Alliance apiga mkwara | Mwanaspoti

BAADA ya kuanza vyema kibarua chake ndani ya Alliance Girls kwa kushinda mechi mbili za Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sultan Juma amesema mechi mbili zijazo dhidi ya Simba Queens na Ceassia Queens ni za kufa au kupona kwani anahitaji alama sita.

Juma aliyerithi mikoba ya Ezekiel Chobanka aliyetimkia Ceassia Queens ya Iringa baada ya kudumu Alliance Girls kwa takribani miaka nane, alianza kwa kishindo akishinda mabao 2-0 dhidi ya Bunda Queens na kuibamiza Mlandizi Queens mabao 5-1.

Matokeo hayo yameipeleka Alliance katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo ikifikisha alama nane. Kabla yake, timu hiyo ilishika nafasi ya tisa kati ya 10 ikivuna alama mbili kwenye mechi tano ikiambulia sare mbili na kupoteza tatu huku ikifunga mabao matatu na kuruhusu tisa.

Kocha huyo aliliambia Mwanaspoti kuwa licha ya Simba Queens na Ceassia kuwa katika kiwango kizuri na kuonekana tishio, lakini zina upungufu na uimara ambao anakwenda kujifungia kuusoma ili kutoa ushindani.

“Timu zote ni ngumu, kila mechi ina mipango yake, kocha natakiwa kujua hilo na kuwasoma kila mpinzani udhaifu na nguvu yake ili kuutumia kukupa faida, hivyo kwenye udhaifu tutautumia na kwenye nguvu tutapambana nao,” alisema Juma.

Akifichua siri ya mwanzo wake mzuri, kocha huyo wa zamani wa Geita Gold Queens alisema wachezaji wamempokea vizuri na wanafuata maelekezo anayowapa, huku akiahidi kuendelea kuboresha upungufu ikiwemo ubutu wa washambuliaji.

Related Posts