MIAMBA ya soka la Afrika, Orlando Pirates ya Afrika Kusini wapo kwenye mipango ya kutafuta mshambuliaji mpya wakati wa dirisha la usajili la Januari, huku ikielezwa kuwa moja ya machaguo yao ni nyota wa Simba, Kibu Denis.
Tangu mwanzoni mwa msimu huu timu hiyo ilihusishwa na washambuliaji kadhaa, lakini ilifanya uamuzi mgumu wa kumrudisha Boitumelo Radiopane aliyekuwa akiichezea kwa mkopo Cape Town Spurs ili kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.
Hata hivyo, Radiopane ameonekana kushindwa kuboresha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, jambo ambalo linaifanya kurudi tena sokoni.
Taarifa kutoka Afrika Kusini zinaonyesha kuwa Kibu anatajwa kama moja ya malengo makubwa ya Pirates na amekuwa akifanya vizuri akiwa na Simba, akifunga mabao muhimu wiki chache zilizopita katika Kombe la Shirikisho Afrika wakati Mnyama akifanya yake dhidi ya CS Sfaxien.
Mwakilishi wa Kibu nchini Afrika Kusini, Gerald Baloyi, amethibitisha kuwa Pirates ni moja ya klabu zinazovutiwa na mshambuliaji huyo ambaye mwanzoni mwa msimu alisaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kusalia Msimbazi.
Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa kuwa Pirates imemuahidi donge nono Baloyi ikiwa atafanikisha dili hilo. Hata hivyo, Pirates pia wamehusishwa na Muzomuhle Khanyi wa Hungry Lions, lakini Kibu anaonekana kuwa kipaumbele.
Pirates wanahitaji mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao na kuleta mabadiliko kwenye safu ya mbele, na Kibu anaonekana kuwa chaguo sahihi.