Unguja. Zaidi ya Sh36 bilioni zilizotolewa na Benki ya Dunia (WB) zitatumika katika mradi wa uhimilivu wa mifumo ya chakula nchini.
Mratibu wa mradi huo upande wa Zanzibar, Sihaba Haji Vuai, amesema mradi huo utasaidia kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wenye tija.
Ametoa kauli hiyo jana Jamanne, Desemba 24, 2024 wakati wa ziara ya kamati ya uongozi ya mradi huo na wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuangalia maeneo yanayohitaji kufanyiwa ukarabati, Cheju wilayani Kati Unguja.
Amesema ziara hiyo inalenga kuwawezesha wajumbe wa kamati kuona utekelezaji halisi uliopo katika maeneo tofauti waliyotembelea na kuchukua hatua za haraka kuhakikisha ukarabati wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji.
“Hatua hiyo inafanyika ili kuharakisha ujenzi wake kuwasaidia wakulima na kufaidika kupitia mradi huo, upatikanaji wa mbegu bora na zinazostahimili ukame na maradhi,” amesema.
Pamoja na kujenga mifumo ya kilimo cha umwagiliaji, maeneo mengine yanayohitaji kufanyiwa ukarabati kupitia mradi huo ni maabara za utafiti wa kilimo Unguja na Pemba zinazomilikiwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Zari), vituo vya wakulima kwenye mabonde ya umwagiliaji maji na ukarabati wa ghala za kuhifadhia mbegu.
Kupitia mpango huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inakusudia kuwainua wakulima hasa katika kuwajengea miundombinu imara itakayowasaidia katika shughuli zao za kiuchumi na uzalishaji, hivyo ziara hiyo itawarahisishia wajumbe waliotembelea maeneo hayo kuona umuhimu wa ukarabati wa miundombinu hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake, Ramadhan Salum Othman, amewapongeza wajumbe hao kufika katika bonde hilo kujionea miundombinu inayohitaji kufanyiwa ukarabati kama mradi unavyoelekeza kukarabati miundombinu ya umwagiliaji maji.
Katika ziara hiyo wajumbe walipata fursa ya kutembelea maeneo ya Mwera, Cheju na Bambi.