Sababu Watanzania kushindwa kumudu mahitaji ya kila siku

Dar es Salaam. Kiwango cha Watanzania wanaoshindwa kumudu gharama za maisha za kila siku kimeongezeka mwaka 2023, Ripoti ya Finscope Tanzania inaeleza.

Ongezeko hili linatajwa na wachumi kuchangiwa na ukosefu wa ajira na shughuli rasmi za kujipatia kipato cha kila siku, sekta zinazokua kuzalisha nafasi kiduchu na ongezeko la watu waliosoma.

Ripoti hiyo inaonyesha mwaka 2017 asilimia 51 ya Watanzania walidai kupata tabu kukidhi mahitaji yao ya kila siku kiwango ambacho kiliongezeka hadi kufikia asilimia 66 mwaka 2023.

Katika ripoti hiyo inaelezwa muktadha wa ukusanyaji wa data unatofautiana kati ya mwaka 2017 na mwaka 2023, kwani wakati utafiti wa mwisho ulipofanyika dunia bado ilikuwa ikikabiliana na athari za Uviko-19 na mdororo wa uchumi.

Licha ya takwimu kuonyesha hivyo, wanaume ndio wanatajwa kuathiriwa zaidi na hali hiyo kulilo wanawake.

Wakijibu swali katika utafiti huo lililohoji, unafanya nini ikiwa huna fedha za kutosha kufanikisha mahitaji yako yote?

Asilimia 20 walieleza wanafanya kazi kwa bidii, asilimia 16 hukopa, asilimia 15 huomba msaada kwa ndugu, asilimia 13 hutumia akiba walizojiwekea, asilimia 12 hubana matumizi, asilimia 11 hufanya kazi za vibarua na asilimia tisa huuza mali walizonazo.

Utafiti huo mwaka 2017 ulionyesha asilimia 56 ya wahojiwa walidai kupunguza matumizi. Katika mwaka 2023 ni Watanzania watatu kati ya 10 waliotaja kuongeza kiwango cha kufanya kazi kwa bidii (asilimia 20).

Akizungumzia ripoti hiyo katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni, mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude anasema ongezeko la Watanzania wanaoshindwa kumudu maisha linaweza kuwa na sababu nyingi, ikiwemo kukosa ajira.

Alisema watu wengi hawana ajira zinazoweza kuwapa kipato kukidhi mahitaji yao na kuendesha maisha.

“Na baadhi wapo kwenye familia tayari, hivyo kufanya uwezo wa kujikimu wao na familia zao kuwa mgumu zaidi,” anasema Mkude.

Wakati hali ikiwa hivi, Mkude anasema siku za usoni, kama Taifa litaanza kuwa na wazee ambao hawajawahi kufanya kazi ya kuwapatia kipato rasmi.

Hali hiyo anasema huwafanya kuwa wategemezi kwa watu wao wa karibu jambo ambalo litaongeza mzigo kwa jamii inayowazunguka katika kuwahudumia na Serikali kwa ujumla.

“Hii ni hali ya kuogofya, hivyo ipo haja ya kuhakikisha miradi ambayo TIC (Kituo cha Uwekezaji Tanzania) wanatangaza kusajiliwa iweze kuzalisha ajira,” anasema.

Uwekezaji katika miradi iliyosajiliwa anayoizungumzia Mkude, taarifa zinaonyesha umeendelea kuongezeka na mwaka huu wa 2024 Tanzania inaweza kuvunja rekodi iliyodumu kwa miaka 11.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri anasema hadi Novemba 29, 2024 kituo kilikuwa kimesajili miradi 800, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni lakini pungufu ya rekodi iliyowekwa mwaka 2013 iliposajiliwa miradi 865.

“Mwaka huu utakuwa mwaka wa rekodi, tangu mwaka 1997 tulipoanza kusajili rasmi miradi mwaka 2013 ndiyo unaoshikilia rekodi lakini sasa kuna uwezekano mkubwa wa kuivunja kutokana na ongezeko kubwa la miradi mwaka huu,” anasema Teri.

Anasema jambo zuri ni kuwa kati ya miradi iliyosajiliwa hadi Novemba 29, ya wazawa ni 260 na zaidi ya nusu ya miradi yote ina ushiriki wa wazawa.

Teri anasema katika miradi iliyosajiliwa mingi ni ya uzalishaji wa bidhaa za mahitaji ya kila siku, sekta ya ujenzi, majengo, uchukuzi, kilimo na utalii.

Mtaalamu wa uchumi, Dk Donath Olomi anasema huenda ongezeko la watu wenye elimu likawa moja ya sababu ya watu kuripotiwa kushindwa kumudu gharama za maisha.

Akielezea suala hilo anasema mtu anapokwenda sekondari anapata mabadiliko katika mtazamo wa maisha hali inayowafanya wasiwe tayari kufanya kazi zilizopo kama vile katika kilimo, uvuvi, upasuaji mbao na vibarua kwenye mashamba.

“Wengi wanajihesabia kuwa wamesoma na sasa wanatafuta vibarua mijini hii inaenda kwa waliomaliza kidato cha sita na vyuo. Wengi hawaoni kama kilimo ni ajira, hivyo ni safari ndefu. Kuongeza watu wanaokwenda sekondari kumechangia kuongeza kiwango cha watu wanaoshindwa kutekeleza mahitaji yao,” anasema Dk Olomi.

Sababu nyingine ni kutokuwapo uchumi jumuishi unaozalisha ajira kwa ajili ya watu wengi ambazo zinaendana na kasi ya ukuaji wa watu unaoshuhudiwa nchini.

Kwa upande wao, wananchi waliozungumza na Mwananchi wanataja kupanda kwa gharama za maisha ni sababu ya wao kushindwa kumudu mahitaji ya kila siku.

Melkidadi Munisi, mkazi wa jijini Dar es Salaam anasema kwa Jiji kama hilo hata kutoka nyumba kwenda sehemu ya kutafuta kipato inahitaji nauli ambayo nayo kwa sasa iko juu.

“Zamani mtu ulikuwa unalipa Sh450 kwenda Kariakoo ukitokea Tandika sasa hivi ni Sh700 maana yake uwe na Sh2,000 kwa ajili ya kufika unapokwenda, tofauti na zamani Sh1,000 ingetosha,” anasema.

Mbali na nauli, anasema  mahitaji ya nyumbani nayo yamezidi kupanda akitoa mfano wa bidhaa kama vile mchele, maharage, sukari na nyama.

“Hiyo nyama yenyewe imekuwa kama anasa hivi sasa, zamani mtu alikuwa akila kuku ndiyo anaonekana ana hela lakini siku hizi wala kuku ndio wasiokuwa na hela kwa sababu kilo moja ya nyama ni kuku wawili,” anasema.

Nyama katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam kilo moja imefikia Sh14,000 huku kuku wa kisasa akiuzwa kati ya Sh6,500 hadi Sh7,000.

Ukosefu wa ajira za moja kwa moja ni jambo linalotajwa na Vicensia Marwa, akisema ni sababu ya watu kushindwa kumudu mahitaji yao.

“Huna kipato cha kueleweka unachoingiza, utapata wapi hela? mbaya zaidi wazazi wote mkiwa ni watu mnaotegemea kupata ajira za muda mfupi, maisha yanakuwa magumu. Hii ni sababu ya watu wengi kuingia kwenye ‘mikopo umiza’ maana mtu anaona hana namna achukue hela atatue shida mwisho wa siku anajikuta anaumia zaidi,” anasema.

Ili kukabiliana na hali hii, Dk Olomi anashauri baada ya kubadilishwa mtalaa wa elimu nchini ni vyema sasa utekelezaji uwe kwa namna inayotakiwa ili uanze kwa kuwaandaa watu waweze kufikia fursa zilizopo, kisaikolojia na kistadi.

“Pia tuweke juhudi katika kukuza sekta zinazobeba watu wengi bila kujali kama zinazalisha ajira rasmi au zisizo rasmi na hizi ni kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara ili ziweze kukua na kuzalisha ajira,” anasema.

Related Posts