Nimekuwa nikiepuka kuzifyatua dini, hasa kinachoendelea, hasara, maudhi, maangamizi, utapeli na wizi wa waziwazi yanayoanza kuzoeleka, nimelazimika kufyatuka na kufyatua vinavyoonekana kutofyatuliwa. Walipokuja wakoloni wa kitasha na wafanya biashara ya utumwa wa kimanga, walituletea dini na utamaduni wao, baada ya kuharibikiwa kwao wakatuharibu tukaharibikiwa.
Kwanza, walifyatua dini zetu kwa kuzitukana, kuzidhalilisha na kuzizika, huku nasi, bila kufikiri wala kuhoji au kustuka, tukazishobokea zao tusijue zitageuka maangamizi yetu tena ya kutendwa na sisi wenyewe.
Pili, walipora majina yetu wakayazika na kutupachika mijina yao tusiyojua hata maana wala mantiki yake, nasi tukakubali.
Tatu, walifyatua kundi dogo la walaji waliotumia na wanaoendelea kutumia dini kutupeleleza na kupeleka habari kwa mabwana zao mbali na kuendelea kutunyonya na kutudhalilisha. Hii, ilisaidia kutuvamia na kututawala kirahisi bila kukoma wala kukomeshwa.
Nne, walipora ardhi, miili na roho zetu kiasi cha kugeuka kanyabwoya.
Tano, walipandikiza, chuki, kiburi na uchonganishi vilivyozaa migongano na hata vita na maafa kwenye baadhi ya jamii kama ilivyo sasa huko Afrika ya Kati (CAR), Msumbiji na Nigeria. Mafyatu waliokuwa wakipendana na kusaidiana, ghafla, waligeuka na kuanza kuchukiana, kuogopana, kushukiana, kuuana, kuibiana, kudanganyana, kutapeliana, kutukanana, na mengine kama hayo.
Wapo walioanza kujiona bora na kuwaona wengine wabovu wakati wote ni wabovu. Leo tunaitana majina mabaya kama vile kafiri, wenye dhambi, na upuuzi mwingine mwingi bila kujua tunajiumiza. Tuko tayari kuuana kwa kutetea imani na mila za wenzetu huku tukizidharau, kuzichukia, na kuzizika zetu wenyewe halafu tunasema ni ukombozi. Ukombozi gani huu?
Baada ya kurogwa na kurogeka vilivyo, ghafla, tuliitwa na kuitana si majina ya kigeni tu bali hata matusi. Mara tuitwe washenzi, wenye dhambi, waliopotea, na wasio na maana wala ustaarabu. Walizika miungu yetu wakasimika na kutukuza yao. Nasi tuliitikia hewala tusijue tunajichimbia kaburi. Ukichunguza kwa undani, kuna ka-ukweli.
Je, vyote hivi kavileta nani kama siyo dini hizi zinazohitaji kukombolewa hata kufyatuliwa zitulipe fidia kwa madhara yasiyoisha zilizotusababishia mbali na kuendelea kutuibia na kutugeuza mazwazwa? Imefikia watu hawafanyi kazi wala kufikiri. Wanangoja miujiza wakati hakuna miujiza kama walivyokubali kugeuzwa mazwazwa bila kuhoji tena kwa miaka mingi. Hawachapi kazi bali kuomba.
Kwanza, kwa nini tulikubali kufyatuliwa kiasi cha kufyatuana hadi sasa? Anayebishia au kulishuku, ajiulize, inakuwaje matapeli tena wajinga na wa kawaida watajirike kwa kuwaibia mafyatu wetu wajinga, wachovu na waliokata tamaa kwa kisingizio cha ima kuwabariki, kuwaombea, kuwatibu, au kufanya miujiza waukate wakati wanakatika?
Siku hizi kaya nyingi za Kiswahili zinaonyesha magonjwa makuu mawili, yaani, dhambi na ulevi. Tuna baa/glosari na nyumba nyingi za ibada kuliko hata mashule na zahati. Je, sisi si wagonjwa hata kama tunajihisi wazima? Hakuna ugonjwa mbaya kama wa akili.
Tumeaminishwa tumerogwa na wale waliorogwa wakaturoga wote tukaishiwa kurogwa na kukorogana bila kujitambua. Haiingii akili mchawi akamponya aliyemroga mwenyewe. Ni ujuha kiasi gani kutegemea tuponywe na wale walioturoga wakati tunapaswa kuwakomboa. Sisi tumerogwa. Dini zimerogwa.
Tunahitaji kujikomboa kifikra kutoka kwenye uchawi uitwao imani. Hebu fikiria kwa makini. Linatokea tapeli moja tena jinga la kutupa linahadaa mafyatu kuwa linaweza kumfufua fyatu aliyekufa wakati lenyewe ni maiti kimaadili na kiakili. Nasi, kwa ujinga na uzwazwa, tunalisikiliza na kuliamini badala ya kulizomea hata kulikong’ota kwa mawe!
Nani kasahau tapeli toka kaya jirani lililojiita Kiboko ya Wachawi? Hii inaonyesha tulivyorogwa tukarogeka. Nani katuroga? Je, ni dini hizi hizi ambazo sasa eti zinatuletea ukombozi wakati zenyewe zinahitaji kukombolewa? Zamani ukimuona kasisi au shehe, unamheshimu. Hii ni kabla ya kuja hawa wa kujipachika hadi unabii.
Tuna kesi kibao za mauaji, ubakaji, ulawiti na uzinzi zinazowahusisha hawa wanaojifanya viongozi wa kiroho wakati ni waroho wa miili na mali zetu. Ni fisi waliovaa ngozi ya kondoo. Tumerogwa tukarogeka hadi kugeuka kondoo wanaochungwa na kuchunwa na fisi hawa. Dini zimerogwa, zimeturoga halafu tunategemea zituponye wakati nazo zinahitaji kuponywa japo kwa kuzifyatulia ukweli huu mchungu.
Umefika wakati wa kuachana na ukondoo, utoto (kutokana na kuzaliwa au kuzalishwa upya), woga na ujinga. Tuseme imetosha. Ukihoji unaambiwa umekufuru. Je, hizi dini nyemelezi za kigeni zilipotutukana kuwa sisi ni washenzi tena wasiostaraabika zilifanya nini kama siyo kufuru na matusi ya nguoni?
Tuliambiwa tuamini bila kuelewa wala kuhoji tukaamini. Tuliogopeshwa kufikiri. Huku ndiko kurogwa tunakomaanisha. Hii ndiyo sababu ya dini kuhitaji ukombozi. Hapa ndipo dini ziliporogwa na kuturoga tukashikilia na kuendelea kurogana kwa kisingizio cha imani na ujinga mwingine mwingi kama ushirikina wa kupakwa mafuta, miujiza, vitambaa, maji ya uzima na upuuzi mwingine. Na hii ndiyo sababu ya kuaminiwa na kugemewa miujiza isiyo lolote wala chochote isipokuwa uongo na utapeli.
Tumalizie. Dini zimerogwa. Zimetoroga. Tunahitaji ukombozi.
Na mkombozi wenu ni Fyatu Mfyatuzi. Niamini nawaambieni. Mimi ni mtenda miujiza pekee anayeishi.
Soma injili yangu ya The Curse of Salvation kitakachochapishwa soon na The Tanzania Educational Publishers Ltd. (TEPU). Hivi nimeishalipia kanywaji haka ninakomalizia?