Beki Mghana aanza tambo Singida Black Stars

BAADA ya kujiunga na Singida Black Stars, beki Mghana Frank Assink amesema hajafanya kosa kujiunga na timu hiyo na anaiona nafasi yake kikosi cha kwanza.

Assink amejiunga na Black Stars kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Inter Allies kwenye nafasi anayocheza anaungana na Tra Bi, Edward Manyama, Keneddy Juma.

Akizungumza na Mwanaspoti, alisema anaheshimu uwezo wa wachezaji wanaocheza ndani ya kikosi hicho, lakini amekuja kuungana nao  kuipambania Black Stars ifikie malengo.

“Mpira ni mchezo wa wazi sitaki kuzungumza mengi. Nikipata nafasi ya kucheza kila mmoja ataona nini kimenileta Tanzania najua Black Stars ina mabeki wengi wazuri na bora, hawanipi shida nimewafuatilia kabla sijafanya uamuzi wa kusaini mkataba,” alisema.

Akizungumzia ligi, alisema hajapata nafasi ya kucheza, lakini amekuwa akiifuatilia na anatarajia ugumu kutoka kwa wenzake na timu pinzani ila amejiandaa kupambana.

Dirisha la usajili limefunguliwa na Singida Black Stars wametoa wachezaji watatu kwa mkopo, Israel Mwenda katua Yanga, Habib Kyomba Pamba na Najim Mussa aliyejiunga na Namungo huku wakiingiza mchezaji mmoja  ilhali taarifa zikieleza imebakiza eneo moja la ushambuliaji.

Singida Black Stars ipo nafasi ya nne baada ya kucheza mechi 15 za mzunguko wa kwanza, imeshinda 10, sare tatu na kufungwa mbili, imefunga mabao 22 huku ikiruhusu nyavu kutikiswa mara 10 na imekusanya pointi 33.

Related Posts