KONA YA MALOTO: Tuhuma za Lissu ‘fedha za Abdul’ na majibu ya Wenje

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, alishusha tuhuma kuhusu mtu anayeitwa Abdul, anayetajwa kuwa mtoto wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwenda nyumbani kwake kumhonga.

Alizungumza kwa mara ya kwanza Iringa Mei 2024 kwenye mkutano wa hadhara. Aliendelea kurejea maneno hayo katika mikutano mingine. Nchi nzima inajua kuwa Lissu alifuatwa kuhongwa fedha na Abdul, akakataa.

Ambacho hakijawahi kusemwa ni kuwa hongo ambayo alitakiwa kupewa lengo lilikuwa nini. Lissu, alishusha tuhuma hizo kipindi ambacho maneno kuwa viongozi wa Chadema “wamelambishwa asali”, yamechukua nafasi tangu chama hicho kilipofanya maridhiano ya kisiasa na CCM mwaka 2022. Mtuhumiwa mkuu wa kulamba asali ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Januari 21, 2023, Mbowe akiwa kwenye mkutano wa hadhara, viwanja vya Furahisha, Mwanza, alitetea maridhiano na kueleza kuwa kuna wenzao ndani ya chama hawaungi mkono.

Yupo mtu angeweza kuunganisha alama na kupata majibu kuwa Lissu aliposema alifuatwa na Abdul kuhongwa, akakataa, alitaka kufikisha ujumbe kuwa yeye siyo kama wengine wanaohongeka. Hafanani na “walamba asali”. Ukifika hapo, jina la Mbowe halipo mbali.

Kilichomponza Mbowe ni kuunga mkono maridhiano. Akayavaa kama beji ya heshima. Maridhiano yalifungua milango na madirisha, hivyo kuruhusu hewa mpya kuingia. Kesi za kisiasa zote zilifutwa, mikutano ya hadhara ilifunguliwa, waliokuwa wamekimbia nchi, walirejea. Unawezaje kumsimanga?

Wengi wanasahau. Mbowe alikaa jela miezi saba, kabla ya kuachiwa, hivyo kufungua milango ya maridhiano. Mbowe, alikuwa akikabiliwa na mashitaka ya ugaidi. Alikamatwa Julai 21, 2021 na kuachiwa huru Machi 4, 2022. Je, alilamba asali ili aachiwe huru na kuunga mkono maridhiano?

Nani hakumbuki? Maridhiano yalifanyika wakati wa uongozi wa Rais Samia. Kabla yake, Ikulu alikuwepo Dk John Magufuli, ambaye hakutaka kutazamana na wapinzani wake wa kisiasa kwa tabasamu. Kesi nyingi za kisiasa, mazingira ya kufanya siasa yalifunikwa na giza, wanasiasa walikimbia nchi. Nani wa kubeza maridhiano? Turejee kwenye fedha za Abdul. Lissu alisema kulikuwa na jaribio la kumhonga. Yupo mtu hakumtaja, ama alimweka kiporo au alimhifadhi kwa sababu zake. Mbio za uenyekiti Chadema zikafanya Lissu amtaje. Ni Ezekia Wenje, Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa.

Nilimsikia Lissu akisema: “Aliyemleta Abdul nyumbani kwangu aje kunihonga, ametangaza kugombea umakamu mwenyekiti na amesema kwa maneno yake mwenyewe anamuunga mkono Mwenyekiti (Mbowe).” Mtajwa ni Wenje.

Neno “afterthought”, hutumiwa sana na wanasheria kwenye mijadala ya kisheria. Lissu ni mwanasheria. Ni kwa nini siku zote Lissu alilihifadhi jina la Wenje? Je, alikaa nalo kama kifungo ili Wenje asiende kinyume chake? Walikuwa na makubaliano ambayo Wenje ameyakiuka? Hakuwa na mpango wa kumtaja ila amekasirika kuona Wenje anamuunga mkono Mbowe dhidi ya yake?

Hutakuwa mbali na ukweli endapo utasema Lissu kumtaja Wenje ni afterthought, yaani fikra zilizofuata baada ya kuona anamuunga mkono Mbowe, ambaye anashindana naye katika mbio za uenyekiti wa Chadema. Yupo anayeamini leo kuwa Wenje na Lissu wana mengi, wakibanwa, wataeleza.

Nilimsikia Wenje akijibu tuhuma dhidi yake. Kwanza hakukataa, isipokuwa amefafanua ukweli upande wake ambao anadai unapindishwa na Lissu. Ukimsikiliza Wenje, unapata jibu moja; hakukuwa na kuhongwa. Habari ya hongo ni tungo nje ya uhalisia. Wenje anasema kuwa alikutana na Abdul kama bahati kwenye shughuli moja, na baada ya utambulisho, moja kwa moja alimhoji: “Kwa nini Serikali ya mama yako haitaki kumlipa Lissu fedha zake za matibabu?” Lissu alishambuliwa kwa risasi nyingi Septemba 7, 2017.

Ni tukio baya kwa kipimo chochote. Ajabu, uliibuka mvutano wa fedha za matibabu ya Lissu. Sera ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), inaelekeza rufaa ya matibabu kwenda nje ya nchi kutolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili. Lissu alishambuliwa kwa risasi Dodoma, akapelekwa Hospitali ya Mkoa ya Dodoma. Kisha, akasafirishwa kwa ndege ya kukodi hadi Hospitali ya Aga Khan, Nairobi, Kenya. Hakupita Muhimbili.

Sababu za kutompitishia Lissu Muhimbili zilikuwa zinajitosheleza kabisa. Alishambuliwa, waliomshambulia hawakuwa wamepatikana. Nadharia zilikuwa nyingi. Hofu kuwa waliotaka kumuua wangeweza kumfuata Muhimbili, ndiyo ilisababisha apelekwe Nairobi.

Msimamo wa Serikali haukubadilika. Kwa kutambua kuwa Lissu alihitaji matibabu na hakuwa na bima, iliitishwa michango nchi nzima hadi diaspora. Mwitikio ulikuwa mkubwa. Tatizo ni moja, ulikosekana uwazi wa michango ya matibabu ya Lissu. Ukiacha Sh200 milioni zilizotangazwa na Mbowe Septemba 23, 2017, hakuna taarifa nyingine. Zaidi, Watanzania hawakuwahi kuambiwa kama fedha walizochanga, zilitosha kugharamia matibabu ya Lissu au kinyume chake. Hivyo, inaleta ukakasi kuona Serikali bado inadaiwa fedha za matibabu ya Lissu. Je, tafsiri ya ile michango ni ipi? Lissu anataka apewe fedha za matibabu ambayo ameshalipiwa na Watanzania? Zingatia, hata Serikali ikilipa ni fedha za Watanzania.

Na je! kwa nini Wenje alianzisha mada ya fedha za matibabu ya Lissu baada ya kutambulishwa kwa Abdul? Nilimsikia Wenje akisema fedha za matibabu ya Lissu zinamhusu kwa sababu naye kuna za kwake. Lissu alichangiwa, ina maana Wenje anataka kurudishiwa fedha alizomchangia Lissu kwa ajili ya matibabu? Wenje anasema Abdul ni muungwana sana, maana alikubali kuongozana naye mpaka Tegeta, nyumbani kwa Lissu.

Swali la jumla ni je, nani anamsingizia mwenzake? Lissu kaamua kumsingizia Wenje kwa sababu ametofautiana naye katika uchaguzi ndani ua chama? Hata hivyo, tuhuma za jaribio la kuhongwa alizitoa kabla ya moto wa uchaguzi ndani ya Chadema. Wenje amechagua kumkaanga Lissu ili kujinasua na kashfa? Wazungu husema “time heals all boo-boos” – “muda hutibu majeraha yote.” Tuwape muda.

Related Posts