Milioni 50 zakwamisha basi Coastal Union

KIASI cha Sh50 milioni zilizotakiwa kulipwa Mamlaka la Mapato Tanzania (TRA), zimedaiwa kukwamisha basi la Coastal Union kutoka bandarini Dar es Salaam na sasa mabosi wapya wanakuna vichwa kukamilisha ndoto ya kumiliki usafiri wa maana wa wachezaji na maofisa wa timu hiyo.

Mzabuni wa Coastal ambaye pia ni mdhamini wa klabu hiyo kutoka kampuni ya Ratco Express, Mohammed Salim ndiye aliyefichua ishu nzima alipozungumza na Mwanaspoti akisema fedha hizo zinatakiwa zilipwe kama ushuru wa basi hilo alizodai ni kubwa kulingana na thamani waliyonunua, hivyo imewalazimu kuiandikia barua TRA.

Alisema wameiandika barua TRA, kitengo cha forodha ili kuangalia uwezekano wa kulipia kwa awali waruhusiwe kulitoa  bandarini jambo ambalo bado wanasubiri majibu.

“Basi la timu aina ya Yutong limekuja, lakini changamoto ambayo imejitokeza ni mfumo wetu wa kodi. Ushuru umekuwa ni mkubwa ukilinganisha na basi zinazotumika kwa biashara tunatakiwa tulipe zaidi ya milioni 50 ambayo ni zaidi ya thamani tuliyonunua, ukilinganisha na Coastal wenyewe ni pesa nyingi mno,” alisema Salim, huku mwenyekiti aliyemaliza muda wa klabu hiyo, Steven Mnguto akisema changamoto ya usafiri kwa klabu na hadi ilipofikia ni ndogo haiwezi kukwamisha maendeleo ya klabu akiahidi kushirikiana na uongozi mpya kuhakikisha usafiri unapatikana Januari 2025.

Mnguto alisema anajivunia kuondoka katika nafasi hiyo aliyohudumu kwa miaka 15 akianzia umakamu mwenyekiti, huku mafanikio yaliyopatikana kipindi chake ikiwemo uwanja uliopo katika mchakato wa ujenzi pamoja na usafiri ambao waliupigania kwa kila namna.

“Changamoto ya usafiri mpaka ilipofikia ni ndogo mno. Tumekwama tu kwa sababu ya ushuru ambao umekuwa ni mkubwa, lakini kuna sintofahamu iliyopo tunayojaribu kuitatua na ikikamilika tutarajie Januari 2025 gari litapatikana. Nitaendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wapya ili hili likamilike,” alisema Mnguto.

Related Posts