Mabehewa 264 ya mizigo treni ya SGR yawasili Dar

Dar es Salaam. Mabehewa ya mizigo 264 yatakayotumika katika reli ya kisasa (SGR) yaliyotengenezwa nchini China yamewasili katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), mabehewa hayo yaliwasili nchini jana Jumanne, Desemba 24, 2024.

Novemba 15, 2024, TRC ilitoa taarifa kwa umma ikieleza meli iliyokuwa imebeba mabehewa hayo iling’oa nanga katika bandari nchini China Novemba 12, 2024 ikijiandaa kwa safari ya kuja Tanzania.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano, Desemba 25, 2024 na TRC, imeeleza kati ya mabehewa hayo, 200 yatatumika kubeba makasha (makontena) na 64 yatabeba mizigo isiyofungwa.

Taarifa hiyo ya TRC iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Fredy Mwanjala imeeleza mchakato wa kuyashusha mabehewa hayo utakapokamilika, hatua itakayofuata ni majaribio yatakayojitika kuyatembeza mabehewa katika reli yakiwa tupu na yakiwa na mizigo.

“Mabehewa hayo yatakuwa yanatembea kwa kasi ya kilomita 120 kwa saa na majaribio yakikamilika, watalaamu wa TRC na wale wa mkandarasi wakijiridhisha mabehewa hayo yamekidhi viwango kwa mujibu wa mkataba, tarehe rasmi ya kuanza kazi itatolewa,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwanjala, shehena ya mabehewa 264 yaliyowasili ni sehemu ya jumla ya mabehewa 1,430 ambayo kwa mujibu wa mkataba yanatengenezwa na Kampuni ya CRRC ya China.

TRC ilianza huduma za SGR kati ya Dar es Salaam na Morogoro Juni 14, mwaka huu na Julai 25 ilianza safari za Dodoma kwa safari za abiria.

Akizindua safari za abiria za SGR Agosti mosi, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuanzishwa kwa treni ya umeme kwa abiria kumekuja na athari katika usafiri wa barabara.

Alisema kupungua kwa idadi ya mabasi barabarani ni jambo litakalokuwa na madhara kwa wafanyabiashara, lakini ni faida kwa Serikali kwa sababu ajali zitapungua.

“Hasara moja ambayo imeanza kuonekana ni kupungua kwa mabasi barabarani. Kwa wafanyabiashara hili ni jambo baya, lakini kwa nchi ni zuri kwa sababu litapunguza ajali na kusaidia kudhibiti usafiri barabarani,” alisema Rais Samia.

Alisema licha ya kupungua kwa mabasi katika baadhi ya maeneo, wasafirishaji bado hawatashindwa kwa sababu baadhi ya maeneo hayajafikiwa na treni hiyo, hivyo wataendelea kufanya biashara katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Rais Samia, athari nyingine zitakazojitokeza ni katika sekta ya usafirishaji wa mizigo, hasa wakati treni itakapokuwa inabeba mizigo. Alisema maeneo mengine bado hayajapata mradi huo, hivyo malori yataendelea kufanya kazi katika maeneo hayo.

Wakizungumza na Mwananchi Novemba, 2024 wachumi, wafanyabiashara na wamiliki wa malori nchini walisema wanatarajia kuanza kwa usafirishaji wa mizigo kwa SGR kutarahisisha biashara kufanyika haraka na kupunguza gharama za bidhaa.

Faida nyingine ya usafirishaji mizigo kwa njia ya treni walisema ni kuepuka foleni inayochangiwa na malori barabarani, kumwezesha mkulima kuuza mazao yake katika masoko anayohitaji kwa haraka bila kupitia kwa madalali.

Kwa mujibu wa TRC, treni ya SGR itakuwa na uwezo wa kubeba mpaka tani 10,000 za mzigo kwa mkupuo, sawa na uwezo wa malori 500 ya mizigo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Augustine Vuma akizungumza kamati ilipofanya ziara TRC, alisema shirika hilo limewaeleza wataanza kusafirisha mizigo kwa njia ya reli kuanzia Januari au Februari, 2025.

“Maana yake hapa tunategemea mapato yataongezeka zaidi ya mara tatu,”alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori nchini (TAMSTOA), Chuki Shaban alipozungumza na Mwananchi wakati huo alisema hakuna athari watakayoipata kwa kuanza kazi treni ya mizigo, akisema kila mbuzi atakula kwa urefu wa kamba yake.

“Umuhimu wa malori uko palepale hata Ulaya bado yapo na yanafanya kazi, tuna wanachama 26,000 nchi nzima na sekta yetu ni kubwa kwa maana hiyo uchumi tunauchangia kwa kiwango kikubwa,” alisema.

Related Posts